TAKUKURU YATANGAZA ZAWADI KWA ATAKAYESAIDIA KUKAMATWA KWA VIGOGO WA SIMBA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) imewataka aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Klabu ya Simba, Zacharia Hans Pope na Frankline Lauwo kujisalimisha katika ofisi zake au kituo cha polisi kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 14, 2018 na naibu mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amedai kuwa Hanspope alitoa taarifa za uongo kuhusu malipo ya kodi.

Amesema Zacharia kwa kushirikiana na washtakiwa wengine Evans Aveva, Geofrey Nyange 'Kaburu' walitoa maelezo ya uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba klabu ya Simba imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Ninah Guangzhou Trading zenye thamani ya Dola 40,577 za Marekani, maelezo ambayo yalikuwa ya uongo kwani nyasi hizo zilinunuliwa kwa dola 109,499.

Kuhusu Lauwo, Mbungo amesema alifanya kazi ya ukandarasi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Simba uliopo Bunju, Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa Sh249, 929,704 wakati akiwa hajasajiliwa katika Bodi ya Makandarasi Tanzania.

"Tumewatafuta kwa njia za siri na uwazi bila mafanikio. Tunawataka kuripoti kituo cha Takukuru au polisi,"amesema Mbungo.

"Mwananchi atakayefanikisha kupatikana kwa watu hawa atapatiwa zawadi.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527