MWANAFUNZI WA DARASA LA TATU APATA UJAUZITO

Serikali wilayani Nkasi mkoani Rukwa, imeagiza kukamatwa kwa wazazi wa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mkinga aliyepata ujauzito kwa kosa la kuandaa mpango wa kumuoza mwanafunzi huyo.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Said Mtanda, wakati akikabidhi pikipiki 28 zenye thamani ya Sh. milioni 98 zilizotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).


Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya mpango wa kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa waratibu kata wa wilaya hiyo.


Alisema katika kijiji cha Mkinga kuna mwanafunzi wa darasa la tatu amepata ujauzito na wazazi wake walikuwa wanaandaa mkakati wa kumuozesha, lakini walishindwa baada ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuingilia kati na kuvuruga mpango huo.


"Naagiza wazazi wote wa mwanafunzi huyo wakamatwe mara moja, mwanafunzi huyo pamoja na aliyempa mimba wafikishwe katika vyombo vya dola, ili sheria ichukue mkondo wake na ninyi waratibu elimu kata tambueni mna jukumu kubwa la kuhakikisha mimba hizi zinakwisha, " alisema.


Mtanda alisema hali hiyo inaonyesha kuwa bado tatizo la mimba ni kubwa kwa sababu katika mwezi uliopita jumla ya wanafunzi 27 walipata ujauzito, hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Misana Kwangula, alisema lengo la serikali kuwapatia pikipiki hizo ni kuwawezesha kutembelea shule zilizopo katika kata zao kwa kuwa walikuwa wanalalamika kuwa hawana vitendea kazi vya kuwawezesha kufanya ukaguzi katika shule wanazozisimamia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527