SPIKA NDUGAI : NI RUHUSA KWA MBUNGE,DIWANI YEYOTE KUHAMA CHAMA CHAKE

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema ni ruhusa kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhama chama kwani huko ndiyo kuimarika kwa demokrasia. 


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua semina kwa ajili ya kamati za uongozi, Wenyeviti na Makamu wenyeviti katika Ofi si ya Bunge Tunguu Wilaya ya kati Unguja alisema hakuna vikwazo wala pingamizi kwa viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo wabunge kuhama vyama.


Alisema kinachofanyika kwa sasa katika matukio ya wabunge kuhama chama na kuhamia kwingine ni mchakato wa kuimarika na kupanuka kwa demokrasia nchini. 


“Ni ruhusa kwa mbunge yeyote kuhama chama chake na kujiunga na chama anachoona kinamanufaa kwake,” alisema. 


Alisema wimbi la viongozi wa vyama vya siasa kuhama vyama hakumaanishi kwamba kutaua demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini.


“Unajua kitendo wanachokifanya ni sawa na kutoka nje kunywa chai na baadaye kurejea ukumbini,” alisema. 


Awali, spika alizitaka taasisi mbili zilizopewa majukumu ya kutunga sheria kushirikiana kwa sababu kazi zao zinafanana. 


Alisema Baraza la Wawakilishi kazi yake kutunga sheria wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano linafanya kazi kama hizo za kuwawakilishi wananchi katika majimbo ya uchaguzi.


“Vyombo vyetu vya kutunga sheria vinatakiwa kushirikiana kikamilifu kwa sababu majukumu yake yanafanana ya kuwakilisha wananchi katika majimbo ya uchaguzi,” alisema. 


Aidha Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid alisema majukumu ya vyombo hivyo ni kuwatumikia wananchi. 


“Ushirikiano wa vyombo hivi ambavyo ni mhimili wa tatu wa dola ni muhimu ikiwa ni Wawakilishi wa wananchi katika majimbo ya uchaguzi,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527