MWIGULU NCHEMBA AKABIDHI NONDO,MIFUKO YA SARUJI KUKARABATI SHULE YA KIBIRIGI

Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba ametoa nondo 46 na kuahidi mifuko 60 ya saruji kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi Kibirigi iliyopo Kata ya Shelui wilayani Iramba.

Amesema hatua ya ujenzi huo ni kutokana na uchakavu ma madarasa yaliyokuwepo hivyo wameamua kujenga upya ili kuwa na muonekano wa kisasa.

Akizungumza na wanakijiji hicho, Dk Mwigulu alisema wanakila sababu ya kuwa na ujenzi wa kisasa kwa sababu zamani wakati majengo hayo yanajengwa hakukuwa na wataalamu wa kutosha.

"Nimeleta nondo hizi pamoja na kuahidi mifuko yote 60 ya saruji inayohitajika ili tuhakikishe tunakamilisha ujenzi huu kuwasaidia watoto wetu,"alisema Dk Mwigulu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibigiri, Sylvester Mang'ena alisema waliona hali mbaya ya madarasa matatu ya shule hiyo hivyo waliibua mradi huo ili kusaidia kuokoa maisha ya wanafunzi hao.

Alisema mradi huo ulianza kwa nguvu za wananchi ambao walikusanya mawe, mchanga, kuchimba msingi na kwamba baadae kila kaya ilichangia Sh 5,000 kwa ajili ya kuchangia ujenzi huo.

"Tunamshukuru Mbunge wetu kwa kutuunga mkono kwa kuchangia nondo na saruji kwa ajili ya kufunga renta na kukamilisha ujenzi tunashukuru kwa kazi hiyo inayoacha alama kwa Iramba yetu," alisema Mang'ena.

Naye, Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo, Chausiku Khatibu alimshukuru Mbunge huyo kwa ujenzi wa madarasa matatu na kumuahidi kufaulu masomo yao.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527