Picha : JESHI LA POLISI SHINYANGA LATOA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA MADEREVA NA WAMILIKI WA VYOMBO VYA MOTO

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limeendesha mafunzo kuhusu masuala ya usalama barabarani kwa wamiliki na madereva wa magari,pikipiki na bajaji ikiwa ni sehemu ya njia za kukabiliana na ajali zinazojitokeza na kusababisha vifo na majeruhi.

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro yamefanyika leo Alhamis Julai 12,2018 katika ukumbi wa Bwalo la Polisi mjini Shinyanga.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro alisema suala la utii wa sheria za barabarani ni jukumu la watu wote hivyo kila mmoja lazima azingatie sheria za barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

"Madereva ni wadau wakuu wa kuzuia ajali za barabarani, nalipongeza jeshi la polisi kwa kuona umuhimu na wadau hawa ili kuwapa elimu hii kwani madereva wakisikiliza na kufanyia kazi elimu hii hakika ajali hazitatokea mkoani Shinyanga",alieleza Matiro.

"Ili kutokomeza ajali,ni vyema jeshi la polisi likaendelea kufanya doria katika barabara kuu, kukagua leseni na kuhakikisha magari yote mabovu hayaiingii barabarani lakini pia kutoa elimu kwa wadau wote wakiwemo wanafunzi",aliongeza Matiro.

Aidha aliagiza mashimo yote katika barabara za mkoa wa Shinyanga yafukiwe huku akiwataka madereva kuacha kuwa wakimya wanapokutana na changamoto hivyo wawasiliane na viongozi wa jeshi la polisi na serikali kwa ujumla ili kutatua changamoto hizo.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule aliwataka watumiaji wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuepuka kuongea na simu barabarani,kuendesha kwa mwendo kasi,kutaka kupita magari bila tahadhari,kulewa na kuendesha magari mabovu.

"Tutaendelea kukamata magari yote mabovu,kukagua leseni,kufanya doria na kutoa elimu kuhusu usalama barabarani kwa makundi yote ili tutokomeze ajali mkoani Shinyanga",alisema Kamanda Haule.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akifungua mafunzo kuhusu usalama barabarani kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya moto yaliyoandaliwa na jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasisitiza waendeshaji wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za barabarani ili kutokomeza ajali mkoani Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akifungua mafunzo hayo. Kushoto ni Afisa Mnadhimu wa polisi mkoa wa Shinyanga Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Lutufyo Mwakyusa, kulia ni Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule akieleza lengo la mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule akiwataka madereva kuacha uzembe barabarani ili kuepuka ajali barabarani
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule akisisitiza kuwa jeshi la polisi litaendelea kuwachukulia hatua za kisheria madereva watakaokiuka sheria za usalama barabarani.Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro . Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Shinyanga SSP Richard George Abwao
Madereva na wamiliki wa vyombo vya moto wakiapa kuzingatia sheria za barabarani ili kutokomeza ajali mkoani Shinyanga.
Kiapo kikiendelea....
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Anthony Gwandu akizungumza wakati wa mafunzo hayo ambapo alisema kila mmoja ana wajibu wa kutii sheria za usalama barabarani.
Wamiliki na Waendeshaji wa vyombo vya moto wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Kulia ni Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule akimuonesha Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ratiba ya mada zinazofundishwa kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya moto ikiwemo magari,pikipiki na bajaji.
Kushoto ni Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Shinyanga SSP Richard George Abwaoakiteta jambo na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga ASP Anthony Gwandu.
Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani  wilaya ya Shinyanga Mkaguzi Msaidizi Emmanuel Pallangyo akitoa mada kuhusu sheria za barabarani
Madereva na wamiliki wa magari,pikipiki na bajaji wakifuatilia mada
Mafunzo yanaendelea
Dereva na mmiliki wa Tax na pikipiki, Omari Gindu akiomba askari wa usalama barabarani 'Trafiki' nao wapewe elimu ya usalama barabarani akidai baadhi yao hawajui sheria hivyo kukamata ovyo madereva na kuchangia kutokea kwa ajali
Mwendesha bodaboda Daudi Salamba akiliomba jeshi la polisi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wadau ili kila mmoja azijue sheria za usalama barabarani
Dereva wa magari/bodaboda Jackson Masengeja akielezea kero yake juu ya baadhi ya askari polisi wanaoendesha bodaboda bila kuvaa kofia ngumu huku wao wakiwa mstari wa mbele kukamata waendesha bodaboda wasiovaa kofia ngumu. 
Mwenyekiti wa waendesha Hiace na Noah wilaya ya Shinyanga Ayub Majenga akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo
Mwenyekiti wa Kituo cha Mabasi mkoa wa Shinyanga  John Mshandete akizungumza wakati wa mafunzo hayo
Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Manispaa ya Shinyanga Wenceslaus Modest akizungumza wakati wa mafunzo hayo
Afisa Bima kutoka Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC),Stella Paul akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya bima kwa vyombo vya usafiri. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani  wilaya ya Shinyanga Mkaguzi Msaidizi Emmanuel Pallangyo
Afisa Mwandamizi kutoka SUMATRA, Bahati Musiba akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya kuondoa baiskeli mjini Shinyanga. Alisema 'huwezi kuondoa baiskeli bila kuleta njia mbadala ni vyema magari yakianza kufanya safari mjini Shinyanga ndipo baiskeli zinaweza kutoka'
Eng. Venance Masanja kutoka TANROADS akitoa ufafanuzi kuhusu mashimo kwenye barabara kuu ya kutoka Mwanza - Shinyanga- Tabora na kueleza kuwa tayari zoezi la kuziba mashimo linaendelea.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527