Thursday, July 12, 2018

WAZIRI NDALICHAKO AKERWA VIFAA VISIVYO NA UBORA KUJIFUNZIA KWENYE VYUO VYA UALIMU

  Malunde       Thursday, July 12, 2018
Waziri wa Elimu Joyce Ndalichako amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya elimu kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na upotevu wa fedha zaidi ya shilingi milioni 800 kwa kununua na kupokea vifaa visivyo na ubora na vingine visivyohitajika kwa matumizi ya kujifunzia katika vyuo vya ualimu wakati shule zinaendelea kukosa vifaa vya maabara kutokana na uharibifu huo.

Maagizo hayo aliyatoa jana baada ya kutembelea Chuo cha ualimu Kasulu TTC na kubaini kuna baadhi ya vifaa vilipokelewa tangu mwaka 2016 vikiwa havina ubora na vingine sio mahitaji ya Chuo hicho, vimehifadhiwa katika maabara ya chuo na havitumiki na vinaendelea kuharibika na kusema kuwa kwa waliofanya manunuzi ya vifaa hivyo wanatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuwa wamefanya uhujumu wa mali za serikali.

Vifaa  hivyo vya maabara vilinunuliwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza viligharimu kiasi cha shilingi milioni 298,074,140/=. na awamu ya pili viligharimu shilingi, 759,999,200/=vifaa vya maabara na vyote vilipokelewa katika vyuo 10 vya ualimu na mpaka sasa hajapokea taarifa yoyote iliyoonyesha vifaa hivyo havina ubora.

Ndalichako alimuagiza Katibu Mkuu kuchukua hatua kwa wale wote waliohusika kununua vifaa hivyo na wale waliovipokea katika vyuo 10 vya ualimu na kupitisha barua ya kupokea vifaa hivyo, na kusababisha wazabuni kulipwa fedha kwa vitu ambavyo havina ubora na kupokea vifaa ambavyo hawavihitaji na kukaa navyo bila kupeleka taarifa wakati wanafunzi wanaendelea kuteseka kusoma bila kuwa na vifaa vya kujifunzia wakati vipo.

"Hamuwezi kupokea vifaa ambavyo hamna uhitaji navyo na vingine havina ubora na kama kweli mlipokea maelekezo kutoka wizarani nitafuatilia.. hapa lazima kuna uhujumu umefanyika, na nyie hamuwezi kuandika barua kwamba mmepokea na sisi tukapitisha malipo bila sababu.. huu ni upotevu na uharibifu wa fedha za umma... nitapita katika vyuo vyote kuangalia vifaa hivi vilinunuliwa na vinafanya kazi nikijiridhisha na taarifa za manunuzi kweli hatutamuhurumia mtu", alisema Ndalichako.

Aidha Ndalichako aliwataka wakuu wa vyuo kuacha kufanya shughuli za ununuzi wa vitu bila kushirikisha bodi ya chuo kwa kuwa vitu vingi vinanunuliwa na bodi haina taarifa jambo ambalo linatia shaka kuwa kuna matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kwa upande wake Boharia wa Chuo hicho Meckisedeck Waziri alisema vifaa hivyo walivipokea kutokana na shinikizo walilokuwa wakipewa kutoka wizarani wakiwalazimisha kupokea vifaa hivyo na baadhi ya vifaa walivyovipokea havina ubora na vingine hayakuwa mahitaji ya chuo.

Mkufunzi wa Masomo ya biolojia katika chuo cha Ualimu Kasulu Yusuph Jonathan alisema vifaa vilivyoletwa mwaka 2016 havikuwa na ubora na vingine havitumiki kufundishia kutokana na mtaala wanaoutumia hivyo vifaa hivyo wamevihifadhi katika stoo ya chuo hicho.

Alisema mahitaji ya vifaa hivyo yalitolewa wizarani wao kama Chuo waliletewa tu vifaa na walipowasiliana na wizara waliambiwa wavipokee na wakalazimika kuvipokea na vifaa hivyo vinaendelea kuwepo stoo na vingine vinaharibika.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Waziri wa Elimu Joyce Ndalichako akizungumza katika Chuo cha Ualimu Kasulu
Waziri wa Elimu Joyce Ndalichako akiangalia vifaa vya kujifunzia visivyo na ubora katika Chuo cha Ualimu Kasulu

Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post