ATUPWA JELA KWA KUUZA NYAMA YA PAKA KWENYE SAMBUSAMtu aliyetuhumiwa kwa kuuza nyama ya paka katika sambusa amehukumwa kifungo cha miaka mitatu na mahakama ya Nakuru nchini Kenya.


Hakimu mkuu Benard Mararo alimhukumu James Mukangu Kimani baada ya kukiri kosa hilo alipowasili katika mahakama hiyo siku ya Jumatatu Juni 25,2018.

Bwana Kimani alishtakiwa kwa kuchinja na kuuza nyama ya paka kwa wateja wake mnamo mwezi Juni 24 mjini Nakuru.

Alishtakiwa kwamba alimchinja paka kwa matumizi ya binadamu kinyume na sheria ya chakula , dawa na kemikali.

Mwanamume huyo alikamatwa Jumapili ambapo inadaiwa alipatikana akimchuna ngozi paka.

Gazeti la Star linasema mwenyewe alikiri kupika sambusa akitumia nyama hiyo.

Taarifa kwenye vyombo vya habari Kenya zinasema mwanamume huyo alikiri kuuza nyama ya paka zaidi ya elfu moja mjini humo tangu mwaka 2012.

Gazeti la Nation linasema aliwaambia wanahabari kwamba alianza 'biashara' hiyo baada ya "kugundua kulikuwa na pengo sokoni".

Alisema huwa anauza pia ngozi za paka na kwamba kwa kila paka hujipatia takriban Sh500 (Dola 5 za Marekani).

"Huwa nawaambia wateja wangu kwamba huwa naipata nyama hii kutoka Gioto (jaa la kutupa taka), lakini huwa hawajui kwamba ni nyama ya paka," alinukuliwa na gazeti la Nation.

Mwanamume huyo alifumaniwa eneo la Railways, Nakuru na alipigwa na umati wa watu kabla ya kuokolewa na maafisa wa polisi na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Ukulima.

Chini ya sheria za Kenya, ni haramu kula nyama ambayo haijakaguliwa na afisa wa afya ya umma, na pia kula nyama kutoka kwa mnyama ambaye haruhusiwi kuliwa Kenya.

Paka si miongoni mwa wanyama wanaoruhusiwa kuliwa chini ya Sheria za Kudhibiti Nyama Kenya.
Chanzo-BBC
Theme images by rion819. Powered by Blogger.