Kimenuka!! POLISI SHINYANGA WAKAMATA SILAHA ZA KIVITA,WAUA MAJAMBAZI WANNE MAKABURINI KAHAMA...ANGALIA PICHA

Watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi eneo la makaburi  ya Kitwana kata ya Busoka tarafa ya Kahama Mjini wilayani Kahama wakati wakijaribu kuwatoroka askari waliokuwa kwenye msako mkali wa kuwatafuta majambazi wanaojihusisha na matukio ya uhalifu katika wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama leo Jumatatu Juni 4,2018,Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule alisema tukio hilo limetokea jana Juni 3,2018 majira ya saa sita na dakika 40 mchana.

Amewataja waliouawa kuwa ni Minani Deo (33) mkazi wa Mabanda Burundi ambaye pia ni muagizaji wa silaha haramu kutoka nchi jirani na Masalamali Paulo (34) mkazi wa Geita ambaye aliachiwa kwa msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia Dkt. John Pombe Magufuli katika gereza la Butimba mkoani Mwanza mwezi Aprili 2018.

Wengine waliouawa ni Hussein Issa Jumanne maarufu kwa jina la Shehe (30) mkazi wa Nyasubi Kahama,Maduhuli Cheyo Maselegu (42) mkazi wa Kigoma Ujiji.

Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo,Kamanda Haule alisema siku ya tukio watu hao walijeruhiwa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za miili yao na kufariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali ya Mji wa Kahama.

“Walikuwa wanaelekea kuwaonyesha askari polisi bastola na bomu moja la kutupwa kwa mkono ‘Hand Grenade) pamoja na washirika wenzao wa ujambazi,wakiwa tayari wameonesha bastola na bomu hilo lililokuwa limechimbiwa chini ya ardhi ndipo walipotaka kuwakimbia askari na askari wakawafyatulia risasi”,alifafanua Kamanda Haule.

“Chanzo cha tukio hilo ni kutaka kuwatoroka askari waliokuwa kwenye msako mkali wa kuwatafuta majambazi wanaojihusisha na matukio ya uhalifu hasa katika wilaya ya Kahama kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Mei 2018”,aliongeza.

Aidha alisema takwimu zinaonesha majambazi hao walikimbilia mkoani Tabora na mara baada ya askari kufika mkoani Tabora wakapata taarifa kuwa majambazi hao wamekimbilia mkoani Kigoma na polisi kufanikiwa kumkamata Masalamali Paulo eneo la soko la Mwanga mkoani Kigoma.

“Baada ya kumkamata na kumhoji aliwataja washirika wenzake watatu wa ujambazi ambao walikimbilia Katumba mkoani Katavi na kufanikiwa kuwakamata wakiwa na silaha ya kivita aina ya AK47 yenye namba UA-2651-1997 iliyokuwa na risasi 30 ndani ya magazine moja ambayo ilipatikana karibu na uwanja wa ndege mkoani Katavi”,alieleza.

Aliongeza kuwa silaha hiyo pia ilikuwa imehifadhiwa pamoja na bastola moja aina ya Browning yenye namba 17569465 ikiwa na risasi 15 ndani ya magazine yake ndani ya shimo.

Alisema katika mahojiano na majambazi hao walikiri kufanya matukio ya uhalifu katika wilaya ya Kahama na mikoa ya Tabora,Geita,Morogoro,Kigoma na Katavi na kwamba miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Mji wa Kahama.

Wakati huo huo,Kamanda Haule alisema mnamo tarehe 28.5.2018 majira ya saa moja na nusu usiku katika mtaa na kata ya Mhungula wilayani Kahama ikipatikana silaha moja aina ya shortgun yenye namba B-15939 iliyokuwa imekatwa kitako na mtutu ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa sulphate ndani ya nyumba ya Malale Kalikisu Malale aliyekuwa anatafutwa na polisi kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Alisema mtuhumiwa alikimbia kabla ya kukamatwa na juhudi za kumtafuta na kumkamata zinaendelea.

Kamanda Haule amewataka wahalifu wote kujisalimisha pamoja na silaha zao ndani ya mkoa au nje ya mkoa na wasipofanya hivyo wataendelea kuwafuatilia sehemu yoyote waliyojificha iwe chini ya ardhi,angani au ziwani ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Mheshimiwa rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli kwa mapenzi yake na wananchi wake,kwa huruma yake aliamua kuwaachia huru wahalifu waliokuwa wamefungwa gerezani akiwemo huyu Masalamali Paulo warudi uraiani,wajirekebishe na washiriki kwenye shughuli za uchumi,sasa baadhi ya hao wahalifu wanauchukulia huu msamaha katika njia ambazo siyo sahihi,hivyo wote walioachiwa kwa msamaha wa rais waendane na maadili mema katika jamii”,alieleza.

“Ndugu wananchi naomba turejee kauli ambayo inatolewa mara kwa mara na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Nyakoro Sirro kuwa uhalifu haulipi, uhalifu hauna nafasi nami pia naungana na kauli ya afande IGP kurudia maneno hayo hayo kuwa kwa sasa uhalifu mkoa Shinyanga hauna nafasi,tunataka wananchi wafurahie matunda ya uhuru,matunda ya uhuru ni amani na utulivu",

"Wananchi wafanye shughuli zao za kiuchumi bila ya kuwa na hofu yoyote ile ya matishio ya kiusalama ili kusudio la kuleta maendeleo katika jamii litimie,natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi mapema”,alisema.

Imeandikwa na Kadama Malunde - Malunde1 blog

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule na askari polisi wakiwa katika eneo la Makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama. Eneo hilo ndiyo sehemu ambapo majambazi yalionesha bastola na bomu lililokuwa limechimbiwa chini ya ardhi kichakani wakataka kuwakimbia askari na ndipo askari wakawafyatulia risasi- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha silaha za kivita walizokuwa nazo majambazi waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi katika makaburi ya Kitwana.
Kulia ni bomu la kutupwa kwa mikono na risasi walizokutwa nazo majambazi hao
Silaha za kivita walizokuwa nazo majambazi hao
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akielezea kuhusu tukio la kukamatwa kwa silaha na kuuawa kwa majambazi hao
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha silaha aina ya AK47 iliyokuwa inatumiwa na majambazi kufanya uhalifu
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha bastola iliyokuwa imefichwa kichakani katika makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha bomu lililokuwa limefichwa kichakani katika makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha silaha aina ya shortgun yenye namba B-15939 iliyokuwa imekatwa kitako na mtutu ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa sulphate ndani ya nyumba ya Malale Kalikisu Malale mkazi wa Mhungula Mjini Kahama aliyekuwa anatafutwa na polisi kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kulia ni Mkuu wa Oparesheni ya kusaka majambazi hao ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga, SSP Amedeus Tesha na Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule (katikati) wakionesha silaha za kivita zilizokuwa zinatumiwa na majambazi kufanya uhalifu katika maeneo ya Kahama na mikoa mingine.
Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Kahama, SP George Bagyemu akifuatiwa na Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule (katikati) na Mkuu wa Oparesheni ya kusaka majambazi hao ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga, SSP Amedeus Tesha wakionesha silaha za kivita zilizokuwa zinatumiwa na majambazi kufanya uhalifu
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akizungumza na waandishi wa habari katika vichaka vilivyopo katika makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama.
Kulia ni Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Kahama, SP George Bagyemu na Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule wakionesha shimo ambamo kulikuwa kumefichwa bomu na bastola katika kichaka kwenye makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akionesha shimo lililokuwa linatumika kuficha silaha za majambazi katika makaburi ya Kitwana wilayani Kahama.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule na askari polisi wakiwa katika eneo la Makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama.Makaburi hayo yamezungukwa na vichaka na miti ambayo imekuwa ikitumiwa na wahalifu kujificha
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akiwa katika mti wa muembe ambao ulikuwa unatumika kama kituo cha majambazi waliouwa katika makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akiwa katika mti uliokuwa unatumika kama kituo cha majambazi katika makaburi ya Kitwana.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akizungumza na wakazi wa mtaa wa Kitwana ambao walidai kuwa wanaona watu wasiojulikana kwenye makaburi hayo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akiwasihi wananchi kuendelea kushirikiana na polisi na kutoa taarifa za kuwafichua wahalifu
Wakazi wa mtaa wa Kitwana wakisimulia matukio ambayo hutokea katika makaburi ya Kitwana
Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga, SSP Amedeus Tesha akitoa rai kwa wananchi kushikiriana na jeshi la polisi katika kufichua wahalifu.
Wakazi wa mtaa wa Kitwana wakiangalia vichaka vilivyokuwa vinatumiwa na majambazi katika makaburi ya Kitwana yaliyopo kata ya Busoka wilayani Kahama.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527