WANAWAKE 2000 KUPATIWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI MKOANI KIGOMA

Katika kutekeleza sera ya Tanzania ya viwanda takribani akina mama 2000 mkoani Kigoma wanatarajia kupata mafunzo ya ujasiriamali yatakayosaidia kuwaimarisha kiuchumi.

Awali akifungua rasmi mafunzo hayo ambayo leo mkoani humo yanatarajiwa kudumu kwa muda wa siku 10 katika halmashauri zote mkoani Kigoma Katibu Tawala msaidizi wa Mkoa wa Kigoma Gaden Machunda  aliwataka akina mama hao kuwa makini kusikiliza mafunzo watakayopata ili kuleta maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla

Aliwasisitiza akina mama kujikita katika ujenzi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2028.

Aidha Machunda aliwataka akina mama kuzingatia misingi ya ujasiriamali pamoja na kuwa na nidhamu na biashara wanazozifanya huku akiwataka wauzaji wa hoteli pamoja na migahawa kuwa nadhifu ili kuwavutia wateja.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya AJ General Company alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanawake pamoja na kusaidia kutekeleza ilani ya serikali ya awamu ya 5 kuelekea ujenzi wa Tanzania ya viwanda.

Alisema kupitia mpango huo wanawake wataweza kuinuka kiuchumi na kupata mikopo isiyokuwa na masharti kama ilivyokuwa hapo awali lakini pia kuwezesha bidhaa zinazozalishwa mkoani Kigoma kupata soko nje ya nchi.

Katibu wa Umoja wa wanawake (UWT) mkoani Kigoma ,Edina Kuguru alisema wao kama viongozi wa wanawake wamejipanga kuhakikisha wanawake wote mkoani humo wanaondokana mfumo wa kuwategemea wanaume kwa kuanzisha warsha na semina mbali mbali za ujasiriamali.

Alisema mikakati waliyonayo ni kutoa elimu ya ujasiriamali na jinsi ya kutumia fedha wanazopewa zinatumika ipasavyo na kuwatafutia masoko kwa kuwa wana mipango ya kuanzisha viwanda vya mihogo na kwa kuwa zao hilo linalimwa sana mkoani Kigoma na ni rahisi kulifanyia uwekezaji.

Hata hivyo alisema Mafunzo ya ujasiRiamali na uwezeshaji kwa wanawake yameanza kufanyika mkoa wa Kigoma kwa kuwa ni mkoa ulioshinda kati ya mikoa mitano iliyopeleka mapendekezo yake na wanaohitaji mafunzo hayo na kukawa na zaidi ya wanawake 2000 waliojiandikisha kushiriki mafunzo hayo.

Mmoja kati ya wanawake wajasiriamali Mkoani Kigoma, Maisala Barakabise alisema wanawake wa Kigoma wanajitahidi kufanya biashara kwa kutumia mitaji yao na wao ndiyo walezi wa familia na ni wathubutu wakiwezeshwa wanaweza zaidi wao wanashughulika na fursa nyingi mkoani Kigoma zinaibuliwa na wanawake na kuzifanyia kazi.

Alisema changamoto wanazokumbana nazo katika kutafuta kipato na kujiondoa katika dimbwi la umasikini ni kuwa na mitaji midogo na hili linasababisha watoto wanapokwenda vyuoni wazazi wanalazimika kuchukua mitaji waliyonayo kuwalipia ada watoto wao waweze kusoma kwa kuwa asilimia kubwa ya Wanawake mkoani Kigoma wanalea familia peke yao.

Kwa upande wake Sakina Kabeza mjasiriamali alisema wanawake wa Kigoma ni wachapakazi na wanajituma kipindi cha nyuma fursa zilikuwa ni chache lakini kwa sasa awamu ya tano imejipanga kikamilifu kutoa fursa kwa wanawake wote na endapo wanawake wa Kigoma wakipatiwa elimu na mitaji wana uwezo wa kufanya vitu vya tofauti sana na kuwaasa wanawake wengine kuchangamkia fursa zilizopo ili kujikwamua na maisha duni.

Aidha aliipongeza taasisi hiyo iliyojitokeza na kutoa elimu na mikopo kwa wanawake mkoani Kigoma na kwamba wanawake wa Kigoma wanajishughulisha na biashara mbalimbali endapo watapatiwa mikopo hiyo itasaidia kuinua uchumi wao na kuanzisha viwanda vya Mihogo na Samaki kwa kuwa ni mazao ambayo wanawake wengi wanajishughulisha nayo fedha hizo zitasaidia kuboresha mitaji na biashara zao.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527