MWALIMU MBARONI KWA KUMTOROSHA MWANAFUNZI NA KUISHI NAYE SIKU NNE

Mwalimu wa Sekondari ya Nyambureti wilayani Serengeti, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumtorosha mwanafunzi wa kidato cha pili kwa zaidi ya siku nne.


Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Juma Shija alikiri kushikiliwa kwa mwalimu huyo na kwamba alikamatwa Mei 2.


Hata hivyo, mwalimu huyo amekana kuwa na uhusiano na mwanafunzi huyo na kwamba hizo ni hila za baadhi ya watu kutaka kumharibia kazi.


Naye mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu alisema mtuhumiwa anadaiwa kumtorosha mwanafunzi huyo wakati wanatoka kwenye michezo ya Umiseta na kukaa naye kwa siku nne.


“Mwalimu hakuonekana kazini kwa siku nne na mwanafunzi halikadhalika, wazazi wakaanza kumtafuta na baada ya kuonekana na kubanwa mtoto alieleza alikuwa kwa mwalimu kwa kuwa ni mpenzi wake,” alisema Babu.


Babu alisema baada ya mtoto kutoboa siri wazazi walikusanyika wakitaka kumshambulia mwalimu huyo hali iliyoufanya uongozi wa wilaya kutuma polisi ili kumnusuru na kumkamata ili aweze kueleza kwa undani.


“Mtoto huyo anadai kuwa walianza uhusiano Oktoba 25, 2017 akiwa kidato cha kwanza na kuwa mke wake akienda masomoni yeye anaendelea naye, kitendo hiki hatuwezi kukivumilia lazima afikishwe mahakamani,” alisema.


Alisema wanaume wakware hawatavumiliwa kwa kuwa wanawaharibia watoto maisha yao.


Mkuu huyo wa wilaya alisema kwa mwaka jana zilikuwapo mimba zaidi ya 25 kwa shule za msingi na sekondari.


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Juma Hamsini amemsimamisha kazi mwalimu huyo kutokana na tuhuma hizo za utovu wa nidhamu na kuitaka polisi kuhakikisha inamfikisha mahakmani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527