WANAFUNZI WALISHWA KINYESI NA MKOJO HAFLA YA KUKARIBISHWA CHUONI

Baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakiteswa katika chuo hicho

Sherehe ya kuwakaribisha wanafunzi wapya katika chuo kikuu cha Msumbiji imezua hisia kali baada ya picha kusambazwa katika mitandao ya kijamii zikioinyesha wanafunzi hao wanavyolazimishwa kunywa na kuoga mikojo na kinyesi.

Kulingana na mwandishi wa BBC Jose tembe mjini Maputo, baadhi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho cha kilimo, misitu na uhandisi cha Unizambeze katikati ya mkoa wa Zambezi pia walinyolewa.

Kulingana na runinga ya kibinafsi ya STV , sherehe hiyo ilifanyika siku chache zilizopita.

Mwathiriwa mmoja , Artemiza Nhantumbo aliambia runinga hiyo kuhusu alivyoteswa.

''Waandalizi wa sherehe hiyo walitukata nywele zetu .Ilikuwa inatisha, ilikuwa haiwezi kuvumilika.Walitulazimisha kula mikojo na kinyesi . Tuliogeshwa na mikojo huku wakifuta pua zetu na vinyesi''.

Mwanafunzi mwengine Quiteria Jorge, alisema kuwa mwanafunzi ambaye alikuwa katika mwaka wa pili aliwatoa katika darasa lao ili kuwafanyia sherehe hiyo ya kukera.

''Walitukata nywele zetu kwa sababu wao wanahisi ni ndefu mno, lakini hatukuweza kufanya chochote, Nililia nikalia hadi nilipofika nyumbani''.

Kisa hicho hakikuwafurahisha wazazi wa wanafunzi hao ambao wamewataka wasimamizi wa chuo hicho kuwachukulia hatua hali wahusika.

Cardoso Miguel ambaye ni mkurugenzi wa elimu ya juu mkoani humo alisema kuwa uchunguzi unaendelea , ''kama tunavyoweza kuona picha katika mitandao ya kijamii ni wazi kwamba tabia hiyo haifai''

Kamati iliobuniwa itachunguza kiwango cha mateso hayo kwa kila mwanafunzi, huku wengine wakirudishwa nyumbani na wengine kufutiliwa mbali .

Sherehe za kuwakaribisha wanafunzi wapya sio rasmi lakini hufanyika sana katika vyuo vikuu nchini humo zikiandaliwa na wanafunzi waliopo katika mwaka wa pili.

Chanzo- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527