TUNDU LISSU AMTOLEA UVIVU SPIKA JOB NDUGAI

Mbunge Tundu Lissu amefunguka na kudai sheria ya uendeshaji wa Bunge halijaweka masharti yeyote ya kupatiwa fedha za matibabu kama alivyo tangaza Spika wa Bunge Job Ndugai hivi karibuni na wala hakuna kifungu chochote kinachozungumzia kibali cha Hospitali ya Muhimbili au cha Rais Magufuli.


Lissu amebainisha hayo usiku wa kuamkia leo kupitia ukurasa wa kijamii zikiwa zimepita takribani siku tatu tokea Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa ufafanuzi juu ya matibabu ya Mbunge huyo kuwa Bunge haliwezi kuidhinisha fedha kwa ajili ya matibabu yake kwa kuwa halijapata vibali vitatu ambavyo vingemuwezesha kupata fedha za matibabu kutoka Bungeni.


"Ukweli ni kwamba kauli ya Spika Ndugai inathibitisha jinsi ambavyo Bunge limepoteza mamlaka na hadhi yake chini ya uongozi wake dhaifu. 


"Hata masuala ambayo Sheria haijampa Rais mamlaka, Spika Ndugai ameyakabidhi. Kauli hiyo ni uthibitisho pia wa jinsi ambavyo Bunge linaendeshwa bila kufuata sheria, kwa chuki na upendeleo wa kisiasa", amesema Lissu.


Pamoja na hayo, Lissu ameendelea kwa kusema "yeye amekwenda India mara nyingi kutibiwa kabla na baada ya kuwa Spika kwa gharama za Bunge. Mimi mbaya wao niliyepigwa risasi nikiwa nahudhuria vikao vya Bunge ninakataliwa matibabu kwa sababu zisizokuwa na msingi wowote. Sio kweli kwamba sikufuata utaratibu, kama maana ya neno hilo ni utaratibu uliowekwa na sheria.

"Kusema nisubiri kibali cha Bunge au cha Muhimbili au cha Rais Magufuli ilikuwa ni kunitakia kifo cha wazi. Katika mazingira ya jaribio la mauaji dhidi yangu, utaratibu pekee uliokuwa unawezekana ulikuwa ni kunihamisha nchini kwa dharura. 


"Nilikuwa nimeumizwa vibaya, mifupa imevunjwa kila mahali, nimepoteza damu nyingi na risasi zimejaa tumboni. Kusema nisubiri kibali cha Bunge au cha Muhimbili au cha Rais Magufuli ilikuwa ni kunitakia kifo cha wazi".


Aidha, Lissu amedai uamuzi wa yeye kupelekwa Nairobi nchini Kenya umetokana na makubaliano ya kikao kilichofanyika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambapo Spika Ndugai na Naibu wake walikuwepo kwenye kikao hicho pamoja na viongozi wengine wa nchi akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu wake Dkt. Ulisubisya Mpoki na Mwenyekiti Mbowe na wabunge kadhaa walihudhuria pia.


"Baada ya kukubaliana kwamba napelekwa Nairobi, ndege ililetwa Dodoma saa sita za usiku. Uwanja wa Ndege wa Dodoma hauruhusu ndege kuruka au kutua baada ya saa 12 jioni. Nani aliyeruhusu ndege iliyonichukua kutua na kuruka saa sita usiku kama hakukuwa na kibali cha Bunge?", amehoji Lissu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527