KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AGOMA KUWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA AFYA KASULU


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Charles Kabeho amekataa kuweka jiwe la Msingi katika mradi Mmoja wa uboreshaji Kituo cha afya cha Kiganamo wenye thamani ya shilingi milioni 500 na kuagiza mradi wa soko la Sofya kufanyiwa marekebisho kati ya miradi saba iliyozinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu kwa madai kuwa kituo hicho kimejengwa chini ya kiwango.

Aidha kiongozi huyo alimuagiza afisa wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha anafuatilia na kuchunguza miradi yote miradi yote ya maendeleo ya ujenzi, maji na afya kwa kuwa miradi mingi haina ubora na thamani iliyotumika katika miradi hiyo haiendani na fedha zilizotolewa na serikali.

Akizungumza jana mara baada ya kukagua mradi wa kituo hicho, Kiongozi huyo alisema Mwenge wa uhuru hautaweka jiwe la Msingi katika mradi wa kituo cha afya hicho kwa kuwa mradi huo umetumia tofali ambazo hazina ubora.

Aidha alimuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufuatilia kasoro hizo kutatuliwa pamoja na kuhakikisha wanachunguza aliyepewa tenda hiyo kama alipatiwa kwa kufuata utaratibu wa manunuzi na kuhakikisha pia wanafanya marekebisho katika mradi wa soko la Sofya katika kufunga bati vizuri ili kuzuia tatizo la wafanyabiashara wanaonyeshewa na mvua.

"Miradi mingi ya maendeleo inakosa ubora kwa kuwa kuna baadhi ya watu wanataka kujipatia asilimia zao niwaombe TAKUKURU mfuatilie miradi ya ujenzi, maji na Afya kwa ajili ya manufaa ya Watanzania kwa kuwa Serikali inatoa fedha kwa ajili ya manufaa ya wananchi lakini baadhi ya watu wasio waadilifu wanatufanya tushindwe kufikia malengo,Mkuu wa wilaya simamia fundi huyo aweze kufanya marekebisho katika mradi wa soko uliowekewa jiwe la msingi na kubainika na baadhi ya changamoto", alisema Kabeho.

Akizungumza wakati akikabidhiwa mwenge na mkurugenzi wa Kasulu Vijijini Mkurugenzi wa Kasulu Mji Fatina Raay alisema Mwenge wa uhuru katika Halmashauri ya Mji utazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba yenye tamani ya shilingi bilioni 3.5 ambapo ni miradi ya sekta binafsi na miradi ya maji na elimu pamoja na afya.

Alisema mradi wa maji katika Kijiji cha Muhunga umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.9 na unatarajia kuhudumia wakazi zaidi ya elfu kumi na mbili na mradi wa pili ni mradi wa uboreshaji wa kituo cha afya cha Kiganamo uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 500 , mradi wa soko la sofya kiasi cha shilingi milioni 198, ujenzi wa vyumba vya madarasa saba katika shule ya Sekondari Muka kiasi cha shilingi 140,000,000 pamoja na mradi wa sekta binafsi wa kutengeneza matofali Murubona na kuzindua klabu mbili za wapinga rushwa na dawa za kulevya.

Nae kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko kanali Hosea Ndagala aliagiza wote wanao husika na masuala ya manunuzi katika mradi huo wa kituo cha afya kuhojiwa na polisi kwa hatua za awali na kumuahidi kiongozi wa mbio za Mwenge kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto zote ziliz jitokeza katika miradi na kumpelekea taarifa baada ya wiki mbili.

Hata hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Kasulu Mji kuhakikisha analifanyia kazi suala hilo na kuwachukulia hatua wale wote watakao bainika kuwa wametumia fedha za serikali kinyume na utaratibu na kuwahakikishia wananchi kuwa serikali itahakikisha miradi yote inakuwa sawa ilikuweza kuwapatia wananchi huduma bora.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527