HALMASHAURI YA BUHIGWE YAPONGEZWA KWA MAJENGO YENYE UBORA

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa charles Kabeho ameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kwa kuzingatia na kujenga majengo yenye ubora kwa kutumia gharama nafuu na kuzishauri Halmashauri zingine kuiga mfano huo.

Akizungumza wakati akikagua mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa vinne na ofisi mbili katika shule ya msingi Kishanga, vilivyogharimu zaidi ya shilingi milioni 100 pamoja na ujenzi wa kituo cha afya na nyumba ya mganga Janda kilichogharimu kiasi cha shilingi milioni 400, ikiwa ni fedha ya ndani Kiongozi huyo wakati akizindua na kuweka jiwe la msingi alisema amefurahishwa na viongozi wa Halmashauri hiyo kwa ubunifu walioufanya na uzalendo baada ya kupatiwa fedha za serikali na kuamua kujenga ujenzi usiotumia gharama kubwa ili kuwasaidia wananchi kupata huduma mapema.

Aidha Kabeho ametoa wito kwa wakandarasi waliopewa zabuni za kujenga miradi katika Halmashauri mbalimbali nchini kufanya kazi kwa kuzingatia viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba yao na kuhakikisha miradi wanayoijenga inakuwa ni yenye ubora.

Amesisitiza kuwa kwa sasa serikali imetoa kipaumbele kwa makandarasi wazawa kufanya kazi ili kuharakisha maendeleo ya nchi yao hivyo wafanye kazi vizuri.

Hata hivyo aliwaagiza wananchi kuhakikisha wanailinda na kuitunza miradi yote ya maendeleo ili vizazi vijavyo navyo viendelee kunufaika na miradi hiyo kwakuwa serikali imejipanga kutatua keto za wananchi kwa kuwawekea huduma za kijamii karibu ikiwa ni pamoja na hospitali, vituo vya afya na shule ili wanafunzi waweze kupata elimu karibu na maeneo wanayoishi.

Wakizungumza mara baada ya uzinduzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kishanga, Bernadetha Samson alisema wanaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kazi kubwa anayoifanya na kuiomba serikali kuendelea kufanya miradi hiyo katika vijiji vingine ili kuondoa kero za upatikanaji huduma kwa wananchi.


Naye John Bhalagaye ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Janda alisema wanaipongeza sana Serikali kwa kuwajengea kituo cha afya kwa kuwa mwanzoni walikuwa wakipata shida kupata huduma za afya katika wilaya ya Kasulu lakini baada ya kituo hicho kikikamilika watakuwa na amani na watapata huduma vizuri.

Kazi nyingine zilizofanywa na Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Buhigwe ni pamoja na kuweka jiwe la msingi Katika ujenzi wa Barabara ya Muzeze Kigogwe, inayotekelezwa na serikali kupitia wakala wa Barabara vijijini (TARURA)kuzindua jengo la kituo cha biashara katika kiiiji cha Buhigwe na kuzindua klabu ya wapinga rushwa katika shule ya msingi Biharu pamoja na uzinduzi wa nyumba bora katika Kijiji cha Muyama.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog 





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527