TENMET KUSHIRIKIANA NA EQUALITY NOW KUPAZA SAUTI ZA WATOTO



Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT), Bi. Cathleen Sekwao (kulia) akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya sauti za watoto juu ya changamoto anuai za ukatili zinazowakabili watoto, maonesho hayo yameandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT) kwa kushirikiana na taasisi ya Equality Now.
Meneja Kampeni wa Taasisi ya Equality Now, Bi. Florence Mashio akizungumza kuhusu unyanyasaji wa watoto hasa kwa mtoto wa kike pamoja na namna ya kuupinga ukatili huo wakati wa maonesho ya ya sauti za watoto juu ya changamoto anuai za ukatilizinazowakabili watoto lililofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

*****
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TenMeT) na taasisi ya Equality Now imekubaliana kufanyakazi kwa pamoja kuhakikisha inapaza sauti za watoto juu ya changamoto mbalimbali za ukatili zinazowakabili hasa watoto wa kike.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika maonesho ya sauti za watoto juu ya changamoto anuai za ukatili zinazowakabili watoto, yalioshirikisha wanachama wa TenMet, Meneja Kampeni wa Equality Now, Bi. Florence Machio alisema matatizo yanayowakumba watoto katika nchi nyingi za afrika yanafanana hivyo kuna kila sababu ya kushirikiana kuyakabili.

Alisema vitendo vya unyanyasaji wa watoto vimekuwa vikiwakatili watoto ndoto zao na  kurudisha nyuma Bara la Afrika kielimu, kwani wengi wamejikuta wanakatishwa masomo  kutokana na ukatili wanaofanyiwa kama vile kutiwa mimba utotoni, kuozeshwa, vitendo vya  ukeketaji na ubakaji dhidi yao.

"Matatizo yanayowakabili watoto nchini Tanzania hayana tofauti na yanayowakabili watoto katika mataifa mengine ya Afrika...hivyo tunapohimiza mabadiliko ya sera na sheria zisizowalinda watoto tuungane kwa pamoja bila kujali unatoka taifa gani," alisisitiza Bi. Machio.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT), Bi. Cathleen Sekwao akizungumza kabla ya kufungua majadiliano kwa wanachama alisema licha ya kushinikiza mabadiliko ya sera na sheria zinazoshindwa kuwalinda watoto sauti za mtoto mwenyewe hazina budi kupazwa ili zisikike kwa jamii nzima.

Aliwataka wajumbe wa mkusanyiko huo kutoka na suluhisho baada ya majadiliano ya pamoja ili kumsaidia mtoto kufikia malengo yake. Alisema wajumbe watapata muda wa kupitia sauti za baadhi ya watoto wakiwa katika changamoto zinazowakabili na kutoka na suluhisho la pamoja kumlinda mtoto.

Mkutano huo mbali na kushirikisha wanachama wa TenMeT ulihudhuriwa pia na wadau pamoja na wawakilishi wa Serikali kutoka idara husika. Equality Now inafanya kazi katika mataifa ya Sierra Leone, Gambia, Mauritania, Kenya, Uganda na Tanzania.
Mwezeshaji na Meneja Programu wa Mtandao wa Elimu Tanzania, (TenMet), Bw. Nicodemus Shauri Eatlawe akizungumza namna ya kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa mtoto wa kike.

Baadhi ya wadau wakiangalia mabango yenye ujumbe mbalimbali zinazohusu kupaza sauti kwa ukatili wa mtoto wakati wa maonesho ya sauti za watoto juu ya changamoto anuai za ukatilizinazowakabili watoto lililofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Afisa Programu wa TenMet, Bi. Alistidia Kamugisha (kulia) akichangia mada kwenye mkutano huo.


Baadhi ya wadau mbalimbali wakichangia mada wakati wa maonesho ya sauti za watoto juu ya changamoto anuai za ukatilizinazowakabili watoto lililofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau kutoka taasisi Binafsi na serikali wakiwa kwenye mkutano uliowakutanisha ili kuangalia namna ya kusaidia mtoto wa kike wakati wa maonesho ya sauti za watoto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527