KINYOZI ATUPWA JELA MAISHA KWA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA 7 AKIOGA BAFUNI KATAVI


MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi  imemuhukumu mkazi wa kijiji cha Sibwesa kilichopo katika wilaya ya Tanganyika , Wilson John (34) ambae ni kinyozi wa nywele kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba.



Mtoto huyo alivamiwa na kubakwa na mshtakiwa wakati akiwa anaoga bafuni nyumbani kwao huku wazazi wao wakiwa sebuleni wakiangalia luniga huku akimtishia kumuua iwapo atamweleza mtu yeyote.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu wa Mahakama hiyo ,Chiganga Ntengwa alisema kuwa mahakama imelidhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashataka pasipo kutia shaka kuwa mshtakiwa alitenda uhalifu huo .

Aliieleza mahakama hiyo kuwa mtu yeyote anayetenda kitendo hicho kama alivyofanya mshtakiwa na kuwa amefanya kosa kinyume na Kifungu cha Sheria namba 130 (1)na (2)e Kifungu cha Sheria namba 131 (3) cha kanuni ya adhabu .

Katika shauri hilo upande wa mashtaka uliita mashahidi sita akiwemo mtoto mwenyewe huku mshtakiwa akina hana shahidi yeyote.

Hakimu Ntengwa alisema kuwa ushahdi uliomtia hatiani mshtakiwa ni uliotolewa na mtoto mwenyewe na uchunguzi wa kitabibu uliothibitisha bila kutia shaka kuwa aliingiliwa kimwili na sehemu zake za siri kuharibiwa pia ushahidi uliotolewa na mama yake mzazi.

Awali Mwendesha Mashtaka , Mwanasheria wa Serikali , Fravian Shiyo alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 24 , mwaka huu saa mbili na nusu usiku nyumbani kwa mtoto huyo ambapo mshtakiwa alikuwa amepanga humo.

Aliongeza kuwa wakati mshtakiwa akifanya uhalifu huo wazazi wa mtoto huyo walikuwa wakiangalia luninga sebuleni kwao.

Kwa mujibu wa Shiyo usiku huo wa tukio mtoto huyo alichukua ndoo ya maji na kwenda bafuni kuoga ambapo mshtakiwa alikuwa amejibanza karibu ya mlango wa bafu ambapo alimweleza mtoto huyo kuwa aingie bafuni kuoga kwamba na yeye (mshtakiwa ) ataingia kujisaidia haja ndogo humo humo.

Ilielezwa kuwa mtoto huyo aliingia bafuni na kuanza koga ambapo mshtakiwa alimvamia na kumziba mdomo kisha akambaka huku akimtishia kumuua endapo atamwambia mtu yeyote.

Shiyo alidai mahakamani hapo mtoto huyo alienda kulala na wenzake chumbani bila kuwafahamisha wazazi wake yaliyomsibu ambapo usiku alisumbuliwa na maumivu makali kwenye sehemu zake za siri.

Ilielezwa kuwa alipozidiwa na maumivu makali alimuomba mtoto mwenzake wa kike waliyekuwa wamelala nae chumba kimoja aende kumuita mama yao mzazi ambaye alipoingia alishtuka kuona godoro alilolalia lilikuwa limelowa damu huku mtoto huyo akilia, ndipo alipomhadithia mama yake kila kitu na alimtaja mshtakiwa.

Hakimu Chiganga Ntengwa kabla ya kusoma hukumu alitoa nafasi kwa mshitakiwa kama anayo sababu yoyote ya msingi ya kuishawishi mahakama iweze kumpunguzia adhabu.

Akijitetea mshtakiwa alidai kuwa hakutenda kosa hilo isipokuwa mama mzazi wa mtoto huyo amemsingizia kwa kuwa alimkatalia kulipa kodi mpya ya chumba ya Sh 40,000/= kwa mwezi ambapo kodi ya awali ilikuwa Sh 20,000/-

Utetezi huo ulipingwa vikali na mwanasheria wa serikali ambaye aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe funzo kwenye jamii kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo na kwa kuzingatia kuwa vitendo vya ubakaji vimekuwa vikitokea mara kwa mara mkoani Katavi .

Baada ya kuzisikiliza pande hizo mbili za mashitaka na utetezi Hakimu Ntengwa alisoma hukumu na kusema mshtakiwa Wilson John mahakama imemuhukumu kutumikia jela maisha yake yote kuanzia jana na kama hakuridhika na hukumu hiyo anayo nafasi ya kuomba rufaa kwenye mahakama nyingine ya ngazi ya juu zaidi.

Hakimu Ntengwa baada ya kusoma hukumu hiyo alimkabidhi Wilison nakala ya hukumu ya kesi hiyo na alikwenda nayo gerezani.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527