WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI WAPEWA ONYO

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewazuia wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kutoka nje ya vituo vyao vya kazi hadi watakapofikia lengo la kukusanya asilimia mia ya mapato ya ndani kabla au ifikapo Juni 30, mwaka huu.

Akihutubia mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (Alat), Mkoa wa Mwanza mjini Nansio, Ukerewe leo , Mongella ameonya kuwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi ambao halmashauri zao zitashindwa kufikia malengo watakuwa wamepoteza sifa za kuendelea kushika nyadhifa zao.

"Hata wenyeviti na mameya ambao halmashauri zao zitakusanya chini ya asilimia mia watasalia kwenye nafasi zao kwa sababu tu wamechaguliwa kwa kura, lakini watakuwa wamedhihirisha udhaifu wao katika usimamizi," amesema Mongella

Amesema hadi kufikia robo tatu ya mwaka wa fedha 2016/17, halmashauri zote nane za Mkoa wa Mwanza zilikusanya mapato kwa asilimia 51 pekee.

"Asilimia 49 iliyosalia lazima zikusanywe ifikapo Juni 30, mwaka huu. Namna mtakavyofanya mimi sijui. Lakini tusije tukaelewana vibaya muda huo ukifika bila makusanyo kufikia asilimia mia moja."

Mkoa wa Mwanza una wilaya saba za Ilemela, Nyamagana, Ukerewe, Kwimba, Magu, Sengerema na Misungwi zenye halmashauri nane.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post