POLISI WATOA ONYO KWA WANACHAMA WA CUF KUKUSANYIKA KWENYE OFISI ZA CUF

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imezuia wanachama wa CUF kufanya usafi katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni kutokana na kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani kutokana mvutano wa makundi mawili.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema ombi la kufanya usafi katika mazingira ya ofisi za chama hicho, liliwasilishwa na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea Aprili 27 mjini Dodoma.

Amesema kutokana na sababu za kiusalama pamoja na mgogoro wa muda mrefu unaoendelea ndani ya chama hicho, Mbunge huyo pamoja na wanachama wengine wanashauriwa kila mmoja kufanya usafi katika eneo lake analoishi au analofanyia kazi.

"Kitendo hicho cha wanachama wa CUF kukusanyika kutoka katika maeneo mbalimbali kwa kigezo cha kufanya usafi kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani na atakayethubutu kujitokeza atachukuliwa hatua za kisheria," amesema Sirro.

Wakati huo huo Kamanda Sirro amesema sakata la watu waliovamia mkutano wa iongozi wa CUF wilaya ya Kinondoni na wanahabari hadi sasa wanawashikilia watu saba akiwemo Mkurugenzi wa Mahusiano wa wa chama hicho, Abdul Kambaya.

Amesema upelelezi wa kesi hiyo, umefanyika vizuri na tayari jalada limefikishwa kwa Mwanasheria wa Serikali kwa ajili ya hatua zaidi ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Jeshi hilo pia limewataka wananchi waliowahi kuibiwa magari yao kujitokeza katika Kituo cha Polisi Mbezi ili kuangalia kutokana,na kupatikana kwa magari matano yanayodaiwa kuibiwa jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527