WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI 'WABESHI" WAMUOMBA MAGUFULI AWAPE MAENEO UCHIMBAJI WASIVAMIE MGODI WA MWADUI


Wachimbaji wa mchanga unaodhaniwa kuwa na madini ya almasi ‘Wabeshi’ wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wameiomba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli iwatengee eneo maalum kwa ajili ya uchimbaji ili waache vitendo vya kuvamia mgodi wa almasi wa Williamson (Williamson Diamonds Ltd).


Wachimbaji hao wa madini ambao wamekuwa wakivamia mgodi na kuambulia kupigwa,kunyanyaswa na hata kuuawa na walinzi wa mgodi huo maarufu mgodi wa Mwadui,walisema yapo maeneo ambayo hayatumiki hivyo ni vyema serikali ikawakatia maeneo ili iwe suluhu ya mgogoro kati yao na uongozi wa mgodi.

Wakizunguza na waandishi wa habari hivi karibuni kwa nyakati tofauti Wabeshi walisema wananchi wanaozunguka mgodi huo wamekuwa hawanufaiki nao kabla na baada ya uhuru hivyo wanaamini serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais Magufuli itatatua kero yao ya muda mrefu.

Walisema vijana wengi wanategemea shughuli ya uchimbaji hivyo wakipewa eneo la uchimbaji wataweza kumudu gharama za maisha ikiwemo kutunza familia zao.

Mmoja wa wabeshi hao Mabula Njile mkazi wa kijiji cha Nyenze kata ya Mwadui Luhumbo alisema endapo serikali itawapatia maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo hawatavamia tena mgodi wa Williamson kwenda kuchimba mchanga unaodhaniwa kuwa na madini ya almasi.

“Tunashuhudia misimamo na maamuzi mazuri yanayofanywa na rais Magufuli katika kuwatetea wanyonge,sisi wabeshi tunampenda rais Magufuli tunaomba asikie kilio chetu,hatuna ajira,tunavamia kutokana na hali ngumu ya maisha,sisi shida yetu ni kupata eneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo hatutaingia tena kwenye eneo la mwekezaji”,alieleza Njile.

Juma Ng’ombeyapi mbeshi kutoka kijiji cha Ng’wang’holo alisema hajawahi kuona kiongozi yeyote wa juu wa serikali akifika katika maeneo yanayozunguka mgodi huo ili kusikiliza kero za wananchi na badala yake baadhi ya viongozi wamekuwa wakishirikiana na uongozi wa mgodi kuwagandamiza wananchi wanaozunguka mgodi huo.

“Hakuna serikali iliyokuja kutusikiliza matatizo yetu,lakini tunaona serikali ya awamu ya tano itatusaidia,tunaomba tupewe eneo la kuchimba ili tusivamie mgodi kwani sasa wananchi tunapigwa,tunateswa,tunaumizwa na wapo ndugu zetu wamepoteza maisha kutokana na kuvamia mgodi”,alieleza Ng’ombeyapi.

“Tuna imani kubwa na rais Magufuli tunataka atusikilize,tunasubiri maamuzi ya rais kwa sababu viongozi wengine wameshindwa kutusaidia na hatuna Imani nao,tumechoka kunyanyaswa katika nchi yetu”,aliongeza mbeshi mwingine Peter Joseph kutoka kijiji cha Ng’wang’holo.

Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Kishapu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo Nyabaganga Talaba alionesha kushangazwa na madai ya wabeshi na kusema wachimbaji hao ‘wabeshi’ wamepewa maeneo ya kuchimba lakini hawataki kuyaendeleza kuyachimba kama wachimbaji wadogo.

“Kwa ujumla wachimbaji hawa hawana vifaa hata ule utaalamu wa kufanya kazi za madini hawana kwa hiyo hata kama wakipewa maeneo ya kuchimba hawataweza kufanya kazi”,alisema Nyabaganga.

“Wanasema wanafanya uchimbaji wa madini lakini uchimbaji wanaoufanya ni wa kuvamia mgodi,na huo wa kuvamia mgodi tumewakataza,kwa sababu ni wizi kwa wizi mwingine,kwa sababu wanaingia siyo kihalali ,wanapora,wanajeruhi hivyo tumewakataza na wala hakuna sheria inayowaruhusu kwenda huko na hilo wanalijua”,aliongeza Nyabaganga.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi wanaozunguka mgodi huo kufanya shughuli zingine badala ya kutegemea mgodi tu kwani mgodi pekee hauwezi kuwaondolea matatizo yao yote.

“Tupo wengi sana,tuna mahitaji mengi,mgodi tu hautatuondolea matatizo yetu,na mgodi tu hautatubadilisha,kuna maisha nje ya mgodi,niwashauri tu wananchi wangu tutafute kitu kingine tunachoweza kufanya badala ya mgodi”,aliongeza Nyabaganga.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Mkazi wa kijiji cha Nyenze kata ya Mwadui Lohumbo akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho
Mchimbaji mdogo wa madini 'Mbeshi' akionesha jeraha kichwani lililotokana na kipigo kutoka kwa walinzi wa mgodi wa Mwadui "Mgodi wa Williamson" baada ya kwenda eneo hilo kuchimba mchanga unaodhaniwa kuwa na madini ya almasi
Mchimbaji mdogo wa madini akizungumza ambapo aliiomba serikali kuwapatia eneo la kuchimba madini
Mchimbaji mdogo wa madini akizungumza mbele ya waandishi wa habari( wengine hawapo pichani)
Mbeshi kutoka kijiji cha Ng'wang'holo kata ya Mwadui Lohumbo akizungumza na waandishi wa habari
Mbeshi akionesha kovu lilitokana na kipigo baada ya kuvamia mgodi wa Williamson
Mbeshi akiomba rais Magufuli kuwapatia eneo la kuchimba ili waache kuvamia mgodi wa Williamson
Mbeshi kutoka kijiji cha Wizunza kata ya Mwadui-Lohumbo akielezea ukatili wanaofanyiwa wachimbaji wadogo wa madini wilayani Kishapu.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post