ONYO KALI LA JPM, KAULI YA WAZIRI MWAKYEMBE BAADA YA KUAPISHWA KUMRITHI NAPE

RAIS Dk. John Magufuli ametoa onyo kwa wamiliki wa vyombo vya habari kwa kile alichosema wanatoa kipaumbele kwa habari zenye nia ovu na kuacha zenye masilahi na taifa.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana akisema kama wamiliki wa vyombo vya habari wanadhani wana uhuru, si kwa kiasi wanachofanya.
Kutokana na hali hiyo, alimtaka Waziri mpya wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeapishwa jana, akachukue hatua akisema kuna wengine walikuwa hawazichukui.
 “Nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari be careful and watch it (kuweni waangalifu) kama mnadhani mna freedom (uhuru) ya namna hiyo not to that extent (siyo kwa kiasi hicho), watu walisema habari za huyu zimezuiwa  lakini utakuta habari za kumtukana zimechapishwa front page (ukurasa wa mbele) sasa kama amezuiliwa si hata za kumtukana msiziandike, kwanini mnaziweka front page.
“Hata kasomeni tu magazeti ya leo (jana), picha yote, heading (vichwa vya habari) ni picha za mtu ambaye alifanya kosa moja kana kwamba kitendo hicho kimefanywa na Serikali au kina support (kinaungwa mkono) na Serikali, page (ukurasa) ya kwanza ya pili huyu anatoa anafanya hivi huyu anatoa hivi ‘that is a story’ (hiyo ndiyo habari),” alisema Magufuli.
Alisema katika vyombo vya habari kumekuwa na utaratibu wa kuzipa uzito mkubwa habari zenye nia ovu kwa Serikali na kuziacha za masuala ya maendeleo.
“Huwezi kukuta mahali wanaandika mambo ya maendeleo, ukikuta ya uchochezi ndiyo yanawekwa, unakuta kwenye TV fulani hivi kila wanapoandamana mahali wakulima au wafugaji ndiyo heading (kichwa cha habari) na inaachiwa muda mrefu sana, hiyo ndiyo story kwao kila kitu chenye nia ya uchochezi fulani fulani wao ndiyo story, sasa Mwakyembe kafanye kazi,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema kama waandishi wa habari wanamchukia mtu, waelekeze chuki zao kwa mhusika si kuichukia Tanzania kwa sababu athari ya vitendo watakavyofanya kwa kuichukia nchi, zitakuwa kubwa kuliko wanavyodhani.
“Moto ukishawaka hakuna wakuuzima, hiyo ni meseji tu kwenu kwamba kalamu zenu mkizitumia vizuri zitawasaidia Watanzania,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli ambaye alimpambanua Dk. Mwakyembe kama mwanasheria mzuri na msomi wa masuala ya habari, alimtaka akafanye kazi kwani Serikali ipo na hawawezi kuiacha ikiangamia kwa sababu ya watu wachache.

Aliongeza kuwa uzalendo umepotea nchini na hali hiyo inasababishwa na viongozi ambao wanawaagiza watu waandike habari za kuitukana Serikali.
“Uzalendo umepotea na unapotezwa na viongozi kwa interest (manufaa) zetu, saa nyingine ndio tumekuwa watu wa kupeleka vitu kwamba kaandike ukaitukane Serikali na wewe upo serikalini, kwa hiyo ni changamoto viongozi tuendelee kuchapa kazi kwa sababu Taifa ni la maana zaidi kuliko masilahi yetu,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza katika uongozi wowote hata ukiangalia misaafu hakuna aliyefanya kazi kwa raha tu kwa kuwa uongozi siku zote ni msalaba.
“Uongozi ni msalaba na ni msalaba kweli, wala si kwa level (kiwango) gani ni kila kiongozi na nyinyi mmeteuliwa kuwa viongozi mtasikia mengi, hizo ndizo changamoto za kazi, unaweza ukawa na mawazo mazuri ukazuiliwa na watendaji wa Serikali ya chini usikate tamaa,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema pia kwamba, kwa sasa nchi ipo katika mwelekeo mzuri hivyo viongozi wanapaswa kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki.
Alisema watu nje ya nchi wanaukubali utendaji kazi wa Serikali iliyopo madarakani lakini japokuwa waliopo ndani wanapingana na utendaji wake.
“Ukienda nje kila mtu ana-appreciate ukirudi huku hakuna anaye-appreciate, tusikate tamaa tufanye kazi kwa ajili ya nchi yetu, siku ikiharibika Tanzania na nyinyi mtaharibikiwa pamoja na hao waliowapanga kuandika mnayoyaandika,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema matatizo yaliyotokea kwenye nchi nyingi ikiwemo Rwanda na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 yalichochewa na kalamu za waandishi.
“Walianza kwa mzaha mzaha hivi, unaweza ukawa unamchukia mtu lakini usiichukie Tanzania, hatuwezi kuacha Serikali ikaangamia kwa sababu ya watu wachache, haitawezekana.
“Watoaji haki katangulizeni Tanzania, majaji mnafanya kazi nzuri katika kutafuta haki, tutengeneze Tanzania yetu, mimi nipo hapa temporary (kwa muda mfupi), makamu wa rais yupo temporary everybody is temporary because the life is so temporary (kila mtu yupo kwa muda mfupi kwa sababu maisha ni mafupi), lakini Tanzania yetu si temporary, itaendelea kuwepo tuilinde hii Tanzania yetu ambayo because it is suppose to be there permanently (kwa sababu idumu),” alisema Dk. Magufuli.
Alisema majukumu yote ya kazi yana lawama, hivyo wasitegemee mazuri hasa katika nchi kama ya Tanzania ambayo ina kikundi cha watu wachache ambao siku zote hulalamika tu badala ya kutafuta majibu ya matatizo yaliyopo.
Taarifa za mitandaoni
Mbali na hilo, Dk. Magufuli alijibu taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba Dk. Mwakyembe hatahudhuria hafla hiyo akisema: “Jana kulikuwa kuna taarifa kwenye mitandao yetu hii ya kijamii.
“Ilivyo ya ovyo walisema Mwakyembe haji kuapa hapa kakataa na mimi nilikuwa nasubiri kwa hamu asije, ikatokea mwingine mheshimiwa Kinana (Katibu Mkuu wa CCM, Abrahman Kinana) kuzungumza kesho (jana) wakati nimemtuma India kwa matibabu na atakaa kule kwa zaidi ya siku 10 na kitu.
“Nikawa nasema Mwakyembe kwa lipi asije lakini ndiyo hali zetu Watanzania, amekuja hapa nimemwita aongee ili wamwone wasije wakasema ni photocopy (wakudurufu),” alisema Dk. Magufuli.
Alisema wapo watu ambao wanatamani Tanzania iangamie bila kujua ni kwa  matakwa ya nani.
Nchi ipo kwenye mpito
Aliwataka viongozi hao wakachape kazi kwa sababu nchi ipo kipindi cha mpito cha kutoka mazoea ya aina fulani kwenda fulani.
Alisema pia katika ziara ya Rais wa Benki ya Dunia (WB), Jim Yong Kim, aliyosema wananchi wanaiponda kupitia mitandao ya kijamii, imesaidia nchi kupata msaada wa Dola za Marekani trilioni 1.74 za miradi ya maendeleo.
“Rais wa Benki ya Dunia ametoa Dola za Kimarekani trilioni 1.74 wakati zilizopo kwenye pipe line (zinazoandaliwa) ni dola trilioni 2.8, sina uhakika kama kuna nchi yoyote wamewahi kufanyiwa hivyo, maji dola za Marekani bilioni 200, bandari dola milioni 250, lakini wananchi wanaongea kama vile hakuna kilichofanyika,” alisema.
Alisema Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT) awamu ya pili, tatu na ya nne zimetolewa dola bilioni 425 wakati vyuo vikuu vya Sokoine Morogoro na  Nelson Mandela Arusha, zimetolewa dola za Marekani milioni 24.
Ahadi za Mwakyembe
Akijibu maswali ya waandishi baada ya kuapishwa, Dk. Mwakyembe aliahidi kuifanyia kazi ripoti iliyotolewa na Kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Nape Nnauye baada ya kituo cha Clouds Media kuvamiwa na askari wenye silaha wiki iliyopita.

“Lile tukio hatuwezi kuli-ignore (kudharau) kwa kuliweka pembeni, kulikuwa na taarifa hizo lakini chanzo ni taarifa za vyombo vya habari ambao ndio walalamikaji, sidhani kama taarifa zimetosha, nahitaji kupata ushahidi unaojitegemea, mlalamikaji hapa ni Clouds na anayeleta taarifa ni Clouds na wenzake, tunachokiona leo ni taarifa ya upande mmoja, nipeni muda ili niweze kukaa na huu upande wa pili ili niweze kupata ukweli wa jambo hili.
 “Nitaongea na upande wa pili ambao umeshindikana kwa mujibu wa taarifa zenu ili kupata taarifa na baadaye ziende ngazi za juu,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema kutafuta taarifa upande wa pili, hauhitaji kamati hivyo hatalifanya mwenyewe kabla ya kuwasilisha ripoti hiyo.
Akizungumzia kuhusu kitendo cha Rais Magufuli kufuta agizo la kuwataka viongozi wa dini, kimila na wengineo wanaofungisha ndoa kutofanya hivyo bila wahusika kuwa na vyeti vya kuzaliwa, alisema hakuwahi kujisikia vibaya kwa tukio hilo.
“Hao wanaoshabikia ni wale wa Richmond tu, mimi sioni shida wala sijajisikia vibaya, kwa sababu Rais ana mamlaka yake kufuta kitu nilichokiagiza sioni kama ni kosa, mimi nilihisi aliona kama ninaenda kasi sana akaamua kunipooza,” alisema Dk. Mwakyembe.
Mbali na Mwakyembe, wengine walioapishwa ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, Katibu Mkuu Ikulu, Alphayo Kidata, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Job Masima, Balozi wa Tanzania nchini Comoro,  Silvester Mabumba na Kamishna wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, Stella Esther Mugasha.
NA AZIZA MASOUD-MTANZANIA DAR ES SALAAM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post