DAKTARI ALIYEMKASHIFU MTUME MUHAMMAD KWENYE MITANDAO YA KIJAMII AKAMATWA ZANZIBAR

JESHI la Polisi Zanzibar linatarajia kumfikisha mahakamani mtu anayedaiwa kumkashifu Mtume Muhammad (S.A.W). 

Mtuhumiwa huyo, Dk. Abdallah Saleh Abdallah (50), mkazi wa Kikwajuni mjini Unguja, baada ya kutoa maneno hayo ya kashfa juzi na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja, Kamishna wa Jeshi la Polisi visiwani hapa, Hamdan Omar Makame, alisema walimtia mbaroni daktari huyo wa binadamu baada ya taarifa zake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo wa Facebook. 

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumkashifu Mtume Muhamad na waumini wa dini ya Kiislamu. 

“Tumemkamata mtuhumiwa na tayari tumeshakamilisha kila kitu, ikiwamo taarifa za upelelelezi. Hivyo kilichobaki ni kumfikisha makahamani tu ili aweze kujibu mashtaka yake,” alisema Kamishna Makame. 

Akiongezea kuhusu ukusanyaji wa taarifa za upelelezi, alisema wamelazimika kumshikilia kijana Ali Juma Makame (30) mkazi wa Michenzani mjini hapa ambaye anatuhumiwa kusambaza video hizo mitandaoni. 

“Tunawanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kutokubali kuyumbishwa na kufanya maandamano kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria, ni bora kujiepusha na jambo hili kwani tayari vyombo vya ulinzi vimeshachukua hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema. 

Kutokana na video hiyo, taasisi mbalimbali za dini ikiwamo Jumuia ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) na Ofisi ya Mufti, zimelaani tukio hilo na kutoa wito vyombo vya sheria kuchukua hatua na kufanya kazi bila upendeleo.

Chanzo-Mtanda blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527