Ileme John Kasili Mtemi Mpya Dutwa wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, akisimikwa rasmi kuwa mtemi wa eneo hilo na wazee wa kimila pamoja na watemi wenzake katika Kijiji cha Dutwa kwenye Mti wa Kitemi uliopo kijijini hapo-Picha na Derick Milton-Simiyunews blog. *******
Baada ya Kifo cha aliyekuwa Mtemi wa Dutwa wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Paschal Mabiti ambaye pia alikuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu wa kwanza tangu mkoa huo kuanzishwa mwaka 2012, hatimaye Septemba 11,2016 eneo hilo limepata mtemi mpya.
Ileme John Kasili ndiye mtemi mpya wa eneo hilo, ambapo alisimikwa katika eneo maarufu la kusimika watemi wa eneo hilo, eneo la mti mkubwa uliko katika kijiji cha Dutwa, kando kando ya Barabara kuu Bariadi-Lamadi, ambapo maelfu ya wananchi wa kijiji hicho walihudhuria sherehe hizo.
Zoezi la kusimikwa kwa Ileme kuwa mtemi mpya wa Dutwa lilianza majira ya saa 4:30 asubuhi nyumbani kwake ambapo alisindikizwa na ngoma za jadi wakiwemo wazee wa kimila, kuelekea katika mti huo na mpaka saa 7:25 mchana zoezi hilo la kusimikwa lilipomalizika.
Baadhi ya wananchi walieleza kuwa kupatikana kwa mtemi mpya, ni faraja kubwa sana kwao na kuongeza kuwa uwezekano wa kupata mvua kubwa na za kutosha kwa mwaka huu ni mkubwa hali itakayosababisha kupata mavuno mengi.
Ileme John Kasili (kushoto) akiwa na mke wake Ngole Kasili, wakisimikwa na wazee wa kimila Kabila la wasukuma, kuwa Viongozi wa Kimila Dutwa wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, zoezi lilifanyika katika mti mkubwa wa kitemi Dutwa.
Mtemi Ileme John Kasili akimwaga maji kuonesha ishara ya kuleta mvua pindi mvua zitakapochelewa katika eneo lake la utawala.
Mtemi wa Dutwa aliyesimikwa Ileme John Kasili (katikati) akirusha Mshale ikiwa ni ishara ya kupambana na maadui mara baada ya kusimikwa kuwa mtemi, huku akiwa amesindikizwa na wananchi wakiwemo wazee wa kimila.
Ileme John Kasili (Katikati) akiwa na mke wake Ngole Kasili wakisindikizwa na wananchi wakiwemo wazee wa kimila kutoka nyumbani kwake Dutwa kuelekea eneo la kusimikwa kuwa mtemi rasmi wa eneo hilo 
Social Plugin