Picha:ASKARI WA JESHI LA ZIMAMOTO WACHAPANA MAKONDE NA WANANCHI BAADA YA KUDAIWA KUPIGA RAIA SHINYANGA

Mwananchi anayedaiwa kupigwa na askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji mjini Shinyanga akiwa amepoteza fahamu

Wananchi wakiwa wamezunguka gari la jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga
 Diwani wa kata ya Kambarage Hassan Mwendapole(aliyeinama kulia) akiwasikiliza wananchi baada ya kutuliza vurugu
Wananchi wakiwa eneo la ofisi za zimamoto
*****

Katika hali isiyokuwa ya kawaida askari wa jeshi la zimamoto na uokokoaji mjini Shinyanga wametwangana makonde kavu kavu na wananchi wanaowazunguka baada ya askari kumshushia kipigo mpaka kupoteza fahamu mfanyabiashara mdogo (Machinga) ambaye hakufahamika jina baada ya kukatiza eneo la ofisi za zimamoto wilaya ya Shinyanga.


Tukio hilo limetokea leo Septemba 26,2016 majira ya saa tano asubuhi ambapo machinga huyo akiwa amebeba nguo zake alipita eneo la jeshi hilo ambalo halina uzio.

Inaelezwa kuwa pamoja na eneo hilo kutokuwa na uzio wananchi hawaruhusiwi kukatisha na wakati machinga huyo akipita ndipo alipokumbana na askari hao na kuanza kupokea kichapo hadi kudaiwa kuzirai.

Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Malunde1 blog kuwa kitendo cha kumpiga raia huyo na kumrukisha kichura chura ndicho kilisababisha wananchi waliokuwa karibu na eneo hilo kupandwa na hasira na kuwavamia askari hao na kusababisha vurugu itokee.


“Wananchi wengi huwa wanapita hapa,leo sijui imekuwaje,wakati adhabu zikiendelea machinga huyo alivulishwa nguo na kubaki na nguo ya ndani huku akimwagiwa maji na kupigwa mitama, muda kidogo tukamuona amezimia”,wameeleza.

“Kufuatia hali hiyo,wananchi tukasogea kuhoji kinachoendelea na kuanza kurushiwa matusi na askari hao,ndipo fujo zilipoanzia ngumi kupigwa kavu kavu huku mawe, chupa zikirushwa ovyo hadi diwani wa kata ya Kambarage Hassan Mwendapole mahali jeshi hilo lililipo alipofika na kutuliza vurugu hizo.

Akizungumza baada ya kutuliza vurugu hizo diwani wa kata ya Kambarage Hassan Mwendapole amelishauri jeshi la zimamoto kutoa elimu kwa wananchi badala ya kutumia nguvu kuwazuia wasipite eneo hilo.

“Ofisi hizi ziko katikati ya watu na hakuna uzio imara,wananchi wamekuwa wakikatiza mara kwa mara pamoja na kwamba kuna vibao vya kuzuia wasipite,wangejikita kuelimisha wananchi,wakikamata basi watoe mkwara kidogo siyo kupiga,kumvua mtu nguo,kumwagia maji,haya yote kivyovyote hayapo kwenye kanuni,huyu raia nimemkuta kapoteza fahamu,kamwagiwa maji na hakuwa anatoka damu",amesema Mwendapole.

Akizungumza na Malunde1 blog,Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Shinyanga Benjamin Inenge amesema huyo raia hajapigwa na kwamba katika eneo hilo la zimamoto wanachokifanya ni kuzuia raia wasikatishe kwa sababu za kiusalama.

“Kilichotokea leo wakati raia huyo anakatisha askari walimzuia na kumwambia arudi alikotokea,akageuka kurudi na kuanzisha vurugu huku akiwatukana askari,kwa sababu eneo hili lina magari pengine angeweza kurusha mawe kwenye vioo,wakaanza kukabiliana naye kwa kumwagia maji,akaanguka chini na kujifanya kazimia,askari wakaanza kumvua viatu”,amesema Inenge.

“Hali hiyo iliwashtua wananchi na kuvamia kituo na kuanzisha vurugu,baada ya hapo tukashirikiana na askari wa jeshi la polisi na askari wa zimamoto kumchukua raia huyo na kumpeleka hospitali,lakini ukweli ni kwamba raia huyo hajapigwa”,ameongeza kamanda Inenge.

Hata hivyo kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Shinyanga Edward Lukuba, amelaani tukio la askari wake kumpiga machinga huyo hadi kupoteza fahamu, na kubainisha kuwa watakaa kikao na kutoa adhabu dhidi yao.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa atazungumzia tukio hilo baadaye baada ya kupata taarifa kwa undani zaidi.

Imeandaliwa na Kadama Malunde na Marco Maduhu- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527