WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATUMBUA MAOFISA WANNE WA MISITU

 
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa misitu wanne, sambamba na kusimamisha shughuli zote za uvunaji wa mazao ya misitu wilayani Rufiji mkoa wa Pwani ili kupisha uchunguzi na kuweka mipango madhubuti ya kusimamia sekta hiyo.


Hatua hizo zilitangazwa jana mjini Rufiji, wakati Waziri Mkuu alipozungumza na watumishi wa wilaya ya Rufiji, kabla ya baadaye kuzungumza na wananchi kwenye ziara yake mkoani Pwani ya kukagua shughuli za maendeleo na kutoa maelekezo kwa watumishi wa sekta ya umma.

Waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Dk Paul Ligonja, Ofisa Misitu Wilaya, Gaudence Tarimo, Ofisa Misitu, Yonas Nyambua na Ofisa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa Wilaya, Suleiman Bulenga.

"Kuanzia leo, nawasimamisha kazi watumishi hawa na geti la Ikwiriri liondolewe mara moja, ni kichaka cha wezi. Pia kazi za uvunaji misitu zisimame zote hakuna kuvuna hadi turatibu upya na kuangalia wapi pa kuvuna wapi si pakuvuna, maana misitu imekwisha na fedha zinaingia mifukoni mwa watu, serikali hainufaiki," alisema Majaliwa.

Aidha, amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo kukusanya magogo yote yaliyopo misituni na kuyapiga mnada .

Aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda wilayani Rufiji, kufanya uchunguzi wa leseni za uvunaji magogo zilizotolewa ili kubaini zilizo halali.

"Rufiji ina sifa mbaya, inaongoza kwa uvunaji misitu bila kufuata taratibu na maofisa misitu wapo, hatuwezi kuendelea hivi,wasimame kazi,wizara itakuja kukagua na wale wasafi watarudi, wachafu njia hiyo nyeupe mwende," alisema Waziri Mkuu.

Majaliwa ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji.

Alisema uvunaji magogo huo, umesitishwa hata kwa wavunaji wenye leseni halali hadi pale uchunguzi utakapokamilika na kuwekwa utaratibu mzuri wa uvunaji kwa faida ya taifa.

Alisema wapo watendaji wanaofanya hujuma kwenye mazao ya misitu kwa kugonga mihuri ya Kilwa kwa magogo yaliyovunwa Rufuji na kisha kuweka fedha mifukoni.

Kuhusu kizuizi cha Ikwiriri, Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Rashid Salum kufuatilia maagizo aliyoyatoa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alipokutana na watumishi wa wizara hiyo.

Alisema katika maagizo yake, alisisita hakuna haja ya serikali kuendelea kuwa na watumishi wasio waadilifu na waaminifu kwa taifa lao, ambao wamepewa majukumu na wao kushindwa kutekeleza kwa kugeuza maeneo ya kazi zao kama vijiwe vya maslahi binafsi.

Aliongeza kuwa, hakuna haja ya kuwa na vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya misitu vingi ambavyo havina tija na badala yake akataka vipungue ili hivyo vichache vifanya kazi kwa ufasaha.

Awali, akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu aliahidi kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Rufiji ikiwemo uhaba wa dawa, watumishi, ununuzi wa kivuko kipya na kuwaahidi kuwekea huduma ya benki.

Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi walibeba mabango yenye ujumbe wa kero mbalimbali, ambazo Waziri Mkuu alilazimika kuwasimamisha watendaji kwenye sekta husika kujibu kero hizo.

Awali, Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa alimwambia Waziri Mkuu kuwa kero kubwa wilayani hapo ni nidhamu mbaya ya watumishi wa umma na kusema wengi sio waadilifu.

Mchengerwa alisema miradi mingi imefujwa ukiwemo wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) na kwamba waliofanya hivyo ni baadhi ya watendaji walioaminiwa na kupewa dhamana na kumtaka Waziri Mkuu kuwawajibisha.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Rufiji kuhakikisha wanapima ardhi na kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuhakikisha wananchi wote wenye maeneo wanapewa hati za umiliki wa maeneo yao waweze kuzitumia kuomba mikopo kwenye taasisi za fedha.
 Imeandikwa na Ikunda Erick-Habarileo Rufiji

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527