Mbunge Wa Chadema Tundu Lissu na Wenzake Wawili Wapandishwa Kizimbani Kwa Uchochezi







Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), amepandishwa kizimbani baada ya kujisalimisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kujibu tuhuma za kuchapisha chapisho la uchochezi lenye kichwa cha habari' Machafuko yaja Zanzibar'.


Lissu alifika mahakamani hapo  saa tano asubuhi, kwa ajili ya kuitikia wito wa kumtaka kwenda kujibu tuhuma za uchochezi zinazomkabili baada ya washitakiwa wenzake wawili akiwemo Mhariri wa Mawio ambalo lilifungiwa kwa muda usiojulikana, Simon Mkina kusomewa mashitaka.


Mbunge huyo na washitakiwa wenzake Mkina na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob, walipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.


Upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi kwa kushirikiana na Salim Msemo, ulidai mahakamani hapo kuna washitakiwa Lissu, Mkina na Mehboob na mshitakiwa Jabir Idrisa bado hawajampata na wamepata taarifa anaumwa.


Kadushi aliomba kumsomea mashitaka Lissu, ambapo alimsomea mashitaka matatu ya kula njama kuchapisha chapisho la uchochezi, kuchapisha taarifa yya uchochezi na kosa la tano ambalo ni mbadala wa kosa la pili la kutishia.


Wakili huyo alidai Lissu na wenzake kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu, Dar es Salaam, walikula njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.


Pia Lissu na wenzake walidaiwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi kati ya wananchi na mamlaka halali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye uchochezi.


Aidha, Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.


Lissu alikana mashitaka hayo, ambapo Hakimu Simba alisema Juni 14, mwaka huu, shauri lilipokuja kwa mara ya kwanza upande wa utetezi ulileta pingamizi juu ya uhalali wa mashitaka wakiomba yafutwe.Kesi hiyo itatajwa Julai 14, mwaka huu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527