UTATA WATANDA WALIOKUFA KWA KUNYONGWA GESTI HUKO MBEYA,HATA MAJINA YALIYOANDIKWA NI FEKI


Hatimaye kitendawili cha watu watatu walionyongwa kisha kuchomwa moto kwenye Gesti ya Mexico mjini Kyela, kimetenguliwa baada ya ndugu kujitokeza na kuwataja kwa majina halisi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema baada ya vyombo vya habari kuandika tukio hilo, ndugu na jamaa wa marehemu walijitokeza na kugundua majina waliyoandika na maeneo wanayotoka ni uongo.


Msangi alisema ndugu wa marehemu baada ya kusoma na kusikia kwenye vyombo vya habari, walianza kuwapigia simu jamaa zao na mmoja wao aligundua kwamba ndugu yake anayeitwa Rogers Mwaka (49), ambaye ni Wakala wa Kampuni ya Vodacom hapatikani na hakuonekana nyumbani.


“Kwa mtandao huo pia tuliweza kufanikiwa kuwapata ndugu wa marehemu wengine, ambao wamewatambua kwa alama na majina yao halisia,” alisema.


Alisema mwanamke aliyeuawa kwenye tukio hilo na kutambuliwa kwa jina la Mariam Hassan, kwa sasa ametajwa kwa majina halisi kwamba ni Zauda Hussein Omary mzaliwa wa Mbarali na mkazi wa Veta jijini hapa wala hatoki Songea.


Msangi alisema marehemu mwingine ametambuliwa kwa jina la Baraka Chaula (27), ambaye ni mdogo wa Zauda kutokana na kuchangia mama, lakini baba tofauti na mkazi wa Mbarali alikuwa akifanya kazi za kilimo na biashara.


Akizungumza kwa uchungu ndugu wa marehemu Zauda na Baraka, aliyejitambulisha kwa jina la Riziki Chaula mkazi wa Mbarali, alisema alifika Kyela baada ya kugundua simu za mdogo wake hazipatikani.


Riziki alisema Zauda ni mke wa Abdallah Malifyuma, anayeishi Mbeya na kwamba alimuaga mumewe kwamba alikuwa akielekea Tukuyu wilayani Rungwe kibiashara.


Mkazi wa Ilomba jijini hapa, Sebastian Amani ambaye alifika Kyela alisema aliamua kupanda gari baada ya simu za Rogers kutopatikana licha ya kuaga kwamba anakwenda Chunya.


Amani alisema chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana na kwamba yamewaweka kwenye wakati mgumu jinsi yalivyotokea.


Jana hiyo, Riziki alishirikana na mume wa Zauda, Malifyuma kuchukua miili ya marehemu hao wawili ilhali Aman ‘akibeba msalaba’ wa kusafirisha mwili wa Rogers.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527