MTOTO AUAWA KWA KICHAPO KISHA KUNING'INIZWA JUU YA MTI BAADA YA KUGOMA KUFUA NGUO ZA MAMAAKE




Mtoto aliyejulikana kwa Jina la Nchambi Tungu(11) Mkazi wa Kata ya Usevya Wilaya ya Mlele ameuawa kikatili na Mama yake mzazi Sado Roketi (26) Mkazi wa Kata hiyo kwa kumpiga na fimbo katika sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumning’iza juu ya mti wa mwembe baada ya kumfunga kamba shingoni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari aliwaambia waandishi wa Habari kuwa tukio hilo na mama kuuawa mtoto wake wa kumzaa lilitokea juzi saa sita mchana kijijini hapo .

Siku hiyo ya tukio marehemu alipewa nguo na mama yake ili azifue hata hivyo mtoto huyo hakuweza kufua nguo za mama yake kwa kile alichodai kuwa alikuwa amechoka .

Kamanda Kidavashari alisema ndipo mama wa mtoto alipokasirika na kuchukua fimbo na kuanza kumpiga kwa kushambulia sehemu mbalimbali za mwili wake huko mtoto huyo akiwa anapiga mayowe ya kuomba msaada na akimsihi mama yake amwachie.

Pamoja na marehemu kuomba msamaha kwa mama yake hakujali ombi la kuombwa msamaha na aliendelea kumpiga kwa kutumia fimbo licha ya mtoto kuendelea kulia.

Kamanda Kidavashari alieleza baada ya kugundua mtoto huyo amefariki dunia kutokana na kichapo alichompa Sado Roketi alimchukua mtoto marehemu huyo na kwenda naye kwenye mti wa mwembe na kisha alimfunga kamba na kumning’iza juu ya mti wa mwembe kwa lengo la kupoteza ushahidi.

Baada ya kumtundika juu ya mti aliendelea kufanya shughuli zake kama kawaida ili watu wasimtilie shaka kuhusiana na mauaji hayo .

Kidavashari alisema Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Sado Roketi na anaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapo kamilika anatarajiwa kufikishwa Mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527