JINSI RAIS MAGUFULI ALIVYOTUMBUA MAJIPU NA KUFUNGA MAKUFULI YAKE MAMLAKA YA BANDARI





Kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupambana na ubadhirifu wa mali ya umma, imezidi kupamba moto baada ya Rais Dk. John Magufuli, kumsimamisha kazi, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, kufuatia ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, jana katika Mamlaka ya Bandari (TPA).

Kufukuzwa kazi kwa Kamishna Mkuu huyo kunafuatia kuthibitishwa kwa taarifa za kupitishwa kinyemela bandarini hapo makontena 349 na kuikosesha serikali mapato ya Sh. billioni 80.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa jana Ikulu na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, nafasi ya Bade inakaimiwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk. Phillip Mpango.

Pamoja na kusimamishwa kazi kwa Kamishna mkuu huyo, Balozi Sefue alisema kuanzia sasa maofisa wote wa TRA hawaruhusiwi kusafiri nje ya nchi hadi uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazo wakabili, utakapokamilika.

Hatua hiyo ya Rais Magufuli inafuatia ziara ya kushtukiza ya Waziri Mkuu aliyoifanya jana katika Mamlaka ya Bandari ambapo alizungumza na viongozi wa mamlaka hiyo na viongozi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Majaliwa alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa watano wa TRA kwa uzembe uliosababisha kupitishwa kwa makontena 349 na kuisababishia serikali hasara ya Sh. Billion 80.

Kwenye mazungumzo yao jana asubuhi, Majaliwa alimtaka Kamishna Mkuu wa TRA, Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Lusekelo Mwaseba kuhakikisha wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kurudishwa serikalini.

Waziri Mkuu aliwataja baadhi ya maofisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.

“Hawa wanasimamishwa kazi...IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi hati zao za kusafiria zishikiliwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Majaliwa wakati akimwagiza IGP, Ernerst Mangu ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo.

Majaliwa pia aliwasimamisha kazi Mkuu wa kitengo cha Tehama, Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa Idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema.

“Hawa wanasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia naagiza wakamatwe na wawe chini ya uangalizi wa polisi,” alisema.
Majaliwa pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile, ambaye alikuwa kwenye kikao hicho, kuhakikisha anapeleka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) haraka iwezekanavyo ili wakakague mifumo ya taarifa na kubaini jinsi ambavyo wizi huo unafanyika.

“Nataka uchunguzi uanze mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye bandari kavu…nataka hayo makontena yatafutwe hadi yajulikane yako wapi na hakikisheni hizo fedha zilizopotea zinarudi serikalini,” alisema.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Awadh Massawe na maofisa mbalimbali kutoka TRA na TPA.

Akijibu maswali ya Waziri Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Bade alikiri kuwa kuna makontena ambayo yamekuwa yakipitishwa bila kulipiwa ushuru na kwamba mchezo huo umekuwa ukifanyika kati ya bandarini na bandari kavu hasa ile iliyoko Ubungo.

BADE ABANWA
Akitoa ufafanuzi, Bade alisema walifanya ukaguzi kwenye bandari kavu moja moja na kukuta makontena 54 yakiwa yameondolewa kabla ya kulipiwa ushuru.

“Hata hivyo tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka na kufikia 327…..tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru)….mmiliki wa bandari kavu ya Ubungo ametakiwa kulipa Sh. billioni 12.6 na hadi sasa ameshalipa Sh. billioni 2.4,” alisema.

Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana majina ya watumishi wanaohusika na wizi huo, Bade alikiri kuwa nayo, lakini kwenye mkutano huo asingeweza kuwa nayo hadi atafutiwe na wasaidizi wake.
Baada ya maelezo hayo, Waziri Mkuu alimuonyesha Kamishna huyo orodha ya makontena 349 yenye taarifa zote hadi namba za magari yaliyobeba mizigo hiyo, lakini hayakulipiwa ushuru.

Kamishna Bade alikiri kwamba orodha hiyo iliyoonyeshwa na Waziri Mkuu kwenye mkutano huo ni ya kweli na ndipo Majaliwa alipokuwa mkali na kutaja majina ya maofisa wanaosimamishwa.

“Kwa utaratibu huu hatuwezi kufika labda baadhi ya watu waondolewe kazini, alisema ,” alisema kisha kutaja maofisa watano waliosimamishwa kazi.

KOVA
Kufuatia agizo la Waziri Mkuu la kuwakamata maafisa wa TRA waliosimamishwa kazi, Kamanda Kova, alisema mpaka sasa jeshi lake linawashikilia maofisa wanne na mmoja kati hayo anaendelea kutafutwa.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527