Aibu !! AFISA MTENDAJI WA KATA AIBA NG'OMBE NA KUMUUZA NA KUTOKOMEA KUSIKOJULIKANA HUKO GEITA

 
Kigogo wa halmashauri ya wilaya ya Geita ambaye ni mtendaji wa kata ya nkome Wilaya na mkoa wa Geita,Peter Francis Kagoma ameikimbia kata yake baada ya kudaiwa kuuza ng’ombe wa wizi kwa thamani ya Tshs 350,000.


Kutokana na hali hiyo,jeshi la polisi Wilaya ya Geita limelazimika kumshikilia Mashauri Magoti(54),mkazi wa kijiji cha Ihumilo kilichopo katika kata hiyo ambaye inaelezwa alishirikiana na mtendaji huyo kumuuza ng’ombe huyo.

Kwa sasa ng’ombe huyo amekamatwa na analindwa na polisi wa kituo kidogo cha polisi Nkome hadi hapo mtuhumiwa namba moja ambaye ni mtendaji atakapopatikana na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Ihumilo ilipoibiwa ng’ombe hiyo Thomas Alila alidai kuwa,desemba 13 walikuta ng’ombe huyo akiwa ametelekezwa na mtu asiyejulikana  nje ya nyumba ya  Mashauri Magoti huku akiwa amefungwa kamba kwenye mti.

Alila anasema walimchukua ng’ombe huyo hadi ofisi ya Mtendaji wa kata ya Nkome ambako walimkabidhi kwa Weo Kagoma na mbele ya mtendaji wa kijiji Charles Buligi kwa lengo la kumtangaza kama utaratibu wa kisheria unavyoelekeza.

‘’Mtendaji huyo alimuomba Magoti ambaye ng’ombe huyo alitelekezwa nyumbani kwake kuendelea kumchunga ng’ombe huyo huku wakitoa matangazo kuona iwapo mwenyewe angepatikana nasi tuliondoka ofisini hapo tukimuacha ng’ombe huyo baada ya kumkabidhi’’alisema Alila.

Hata hivyo katika hali isiyotarajiwa,desemba 23 mwaka huu ofisa mtendaji huyo,alimuuza ng’ombe huyo kwa thamani ya Tshs 350,000/=,na baadaye ng’ombe huyo alikamatwa na wananchi akiwa mbioni kuchinjwa.

‘’Baada ya wananchi kumkamata ng’ombe huyo walinitaarifu na nilipofika eneo la tukio mnunuzi alikimbia na sisi kama viongozi tulimchukua ng’ombe huyo na kumfikisha katika kituo cha polisi cha nkome aliko hadi sasa’’alisema Alila.

Akizungumza na Malunde1 blog  kabla ya kukamatwa,mchungaji wa ng’ombe huyo Magoti ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi,alikiri mtendaji Kagoma kumuuza ng’ombe huyo nay eye kupatiwa mgao wa Tshs 100,000 kama malipo ya kumlinda ng’ombe huyo kuanzia alipokutwa ametelekezwa nyumbani kwake hadi siku ya kuuzwa.

Naye Kagoma alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi simu iliita bila kupokelewa.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Nkome  OCS E 5147 D/CPL Mtawa mbali na kukiri mtendaji huyo kukimbia na ng’ombe huyo kushikiliwa kituoni hapo alimtaka mwandishi wa habari hizi kumtafuta kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo ambaye ndiye msemaji mkuu wa jeshi hilo.

‘’Ni kweli ng’ombe yupo kituoni na mtendaji baada ya kumuita afike kituoni amedai amepatwa dharula ya ghafla na leo siku ya 4 kila ukimpigia simu anadai yuko visiwa vya wilaya ya Sengerema lakini ukitaka taarifa kamili mtafute kamanda wa polisi mkoa wa Geita huyo ndiye msemaji wetu’’alisema OCS Mtawa.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ali Kidwaka alikiri kupokea malalamiko hayo dhidi ya mtendaji huyo na kuahidi kufuatilia.

Na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita 

Bonyeza hapa Tukupe habari zote mara moja zikitoka "HABARI" VITUKO "MAPENZI"MAGAZETI,UDAKU>
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba  +255 688 405 951

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527