Makovu ya Uchaguzi !! CHADEMA YAIBWAGA CCM MAHAKAMANI GEITA


Mahakama ya Wilaya ya Geita mkoani Geita imetupilia mbali shauri la madai ya uchaguzi wa serikali ya mtaa wa Nyantorotoro “A”  na kuamuru mlalamikaji ambaye ni mgombea wa  Chama Cha Mapinduzi(ccm) kulipa gharama za kuendesha shauri hilo.


Akisoma hukumu hiyo leo mahakamani ,Hakimu  mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Geita Desdery  Kamugisha alisema mlalamikaji amekosea madai yake kwa kuomba mahakama ibatilishe uchaguzi wa mtaa wa Nyakagwe na kwenye maelezo  ya shauri analalamikia uchaguzi wa mtaa wa Nyantorotoro “A”.


Awali mlalamikaji ambaye alikuwa mgombea wa mtaa huo kupitia Chama Cha Mapinduzi(ccm) Martine Lunzari alidai aondoe malalamiko yake mahakamani kwa muda ili akafanye marekebisho kwenye hati zake za madai.


Aidha alikiri mahakamani hapo kuwa hati zake za madai zilikosewa kwa kuandika madai ya mtaa wa Nyakagwe wakati yeye aligombea mtaa wa Nyantorotoro “A” na kumboa mahakama iondoe hati hizo ili akafanye marekebisho ili aandike mtaa kwa usahihi.


Akijibu hoja hizo,wakili wa Chadema Jimbo la Geita Bernard Otieno aliambia mahakama hiyo kuwa mlalamikaji amekosea kufungua shauri hilo na amekosea msingi wake na amefunga mikono ya mahakama hiyo kwa kumlalamikia mgombea wa mtaa wa Nyakagwe badala ya mtaa wa Nyantorotoro “A” na kuiomba mahakama itupiliwe mbali shauri hilo.


Otieno alisema kuwa, mahakama itupilie mbali shauri hilo kwa sababu kuruhusu shauri hilo liendelee ni kukiuka sheria na taratibu hivyo mahakama imefungwa mikono na haina budi kuifuta na kuamuru kulipa gharama za kesi hiyo.


Akitoa hukumu hiyo hakimu Kamugisha alisema kuwa, kuruhusu mlalamikaji kufanya marekebisho katika hati hiyo ya madai itakuwa ni kuruhusu kufuta hoja ya msingi wa shauri lenyewe,hivyo akatupilia  mbali shauri hilo na kuamuru kulipa gharama za shauri hilo.


Akizungumza na Malunde1 blog Wakili wa Chadema Jimbo la Geita Otieno alisema kuwa shauri hilo lilikuwa na makosa makubwa na ya kisheria na kumpongeza hakimu kwa kujielekeza vizuri kwa mujibu wa sheria.


Katibu wa Chadema Jimbo la Geita Mutta Robert,alisema kuwa kesho asubuhi ataenda mahakamani na wakili wao kupeleka madai ya gharama za shauri hilo.


“Kesho mapema tunaenda mahakamani na wakili wetu kusajili madai ya gharama za shauri hilo baada ya kushinda mahakamani,pia tunaendelea kujipanga na wakili wetu kupangua mashauri mengine mawili yaliyobaki”


Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika 14 Desemba,2014 katika Halmashauri ya mji wa Geita Chadema iliishinda vibaya CCM baada ya Chadema kuibuka mshindi katika mitaa 34 na ccm kupata 24 na kati ya mitaa hiyo,mitaa 4 ccm waliipata kwa kuweka pingamizi na kupita bila kupingwa.


Matokeo hayo yalionesha kuwachanganya viongozi wengi wa ccm na kuamua kufungua madai mahakama ya wilaya.
Mpaka sasa waliokuwa wagombea wa ccm katika mitaa 3 wamepeleka mashtaka ya madai mahakamani.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita 


Bonyeza hapa Tukupe habari zote mara moja zikitoka "HABARI" VITUKO "MAPENZI"MAGAZETI,UDAKU>
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba  +255 688 405 951

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527