Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, amesema maadili, uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma ni msingi wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuendelea kuwa na imani na Serikali.
Amesema tabasamu la wananchi linalokusudiwa katika utoaji wa huduma za umma haliwezi kupatikana iwapo watumishi wataendelea kujihusisha na vitendo vya rushwa, urasimu, matumizi mabaya ya madaraka na lugha zisizo na staha wanapowahudumia wananchi.
Qwaray ameyasema hayo leo November 26,2026 jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao kazi cha saba cha kubadilishana uzoefu baina ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, taasisi zinazosimamia maadili ya utendaji na mamlaka zinazosimamia maadili ya kitaaluma.
Amesema kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kupima mafanikio ya uongozi kwa tabasamu za wananchi inapaswa kutafsiriwa kupitia namna watumishi wa umma wanavyotekeleza majukumu yao, ikiwemo kutoa huduma kwa wakati, kuondoa urasimu na kuzingatia haki bila kudai rushwa.
“Tunaporuhusu ukiukaji wa maadili katika ofisi zetu, ile tabasamu aliyosema Dk. Samia Suluhu Hassan itapotea. Mwananchi kupata huduma siyo kutoa rushwa, na sisi kutoa huduma ni wajibu wetu, siyo mpaka upewe rushwa,” amesema.
Ameongeza kuwa watumishi wa umma wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanazostahili bila kubaguliwa, kuzungushwa au kukumbana na vikwazo vinavyosababishwa na mienendo isiyozingatia maadili.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, vitendo vya rushwa, uvujishaji wa siri za Serikali, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, hujuma dhidi ya miradi ya maendeleo, upendeleo na matumizi ya lugha zisizo na staha ni miongoni mwa viashiria vya ukiukaji wa maadili vinavyoendelea kujitokeza katika utumishi wa umma.
Amesema hali hiyo inahitaji taasisi zinazosimamia maadili kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kushughulikia ukiukaji wa maadili katika maeneo mbalimbali ya kazi.
Amesisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kutambua kuwa namna anavyotekeleza majukumu yake inaakisi Serikali, kwa kuwa shughuli za Serikali hutekelezwa na watumishi wa umma kwa niaba ya Rais, kama inavyoelekezwa katika Ibara ya 35(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali katika usimamizi na utoaji wa huduma, lakini hatua hizo zinapaswa kwenda sambamba na uadilifu wa watumishi ili wananchi wanufaike na maboresho yanayofanyika.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora imepanga kuanzisha katika mwaka huu wa fedha zoezi la ujumuishaji wa programu za maadili katika taasisi za umma, kwa lengo la kuhakikisha mafunzo na elimu ya maadili vinawafikia watumishi katika maeneo yao ya kazi.
Amezitaka taasisi zinazosimamia maadili ya kiutendaji na mamlaka za maadili ya kitaaluma kuweka kipaumbele katika kuanzisha programu zitakazojenga utamaduni wa uadilifu, huku viongozi wakitakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika tabia, mienendo na maamuzi yao.
Aidha, amehimiza taasisi hizo kuhakikisha miongozo na nyaraka za maadili zinapatikana kwa urahisi kupitia tovuti rasmi, kuweka mifumo rafiki ya kupokea na kushughulikia maoni na malalamiko ya wananchi, pamoja na kuwajengea watumishi uwezo kuhusu kanuni za maadili ya utumishi wa umma.
Amesema pia matumizi ya mifumo ya Serikali mtandao yanapaswa kuimarishwa ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji, akisisitiza umuhimu wa kila mtumishi kuwa na anwani rasmi ya barua pepe ya kikazi kwa ajili ya mawasiliano ya kiofisi.
Amesema Tume ya Utumishi wa Umma inatarajiwa kuratibu kikao cha nane, kufuatia utaratibu huo wa kubadilishana majukumu ya maandalizi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Patient Ntwina, ameipongeza Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuandaa kikao hicho, akisema inatoa fursa kwa taasisi husika kubadilishana uzoefu na kupata mbinu za kuboresha usimamizi wa maadili katika maeneo yao ya kazi.
Ntwina amesema maelekezo yaliyotolewa yanapaswa kugeuzwa kuwa maazimio na kutekelezwa katika taasisi husika ili kuhakikisha elimu na uzoefu unaopatikana kwenye vikao hivyo unaonekana kwa vitendo.
Amesisitiza umuhimu wa washiriki kuwasilisha kwa waajiri wao taarifa za masuala yaliyojadiliwa na maazimio yaliyofikiwa ili kuongeza wigo wa manufaa ya kikao hicho kwa watumishi wengine wa umma.
Kikao hicho ni cha saba tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao hivyo mwaka 2018, ambapo uratibu wake hufanyika kwa kupokezana miongoni mwa taasisi shiriki.
Aidha Kikao cha tano kiliandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), huku cha sita kikiandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT)na vyote vikifanyika Dodoma.
Vilevile Tume ya Utumishi wa Umma inatarajia kuratibu kikao cha nane kwa tarehe itakayokuwa imekubaliwa kupitia maazimio ya kikao hicho.







TAFUTA HABARI
Social Plugin