Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MASWI AWASILI RASMI OFISI NDOGO ZA TAMISEMI, AHAIDI USHIRIKIANO KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI


Na: OWM–TAMISEMI, Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Bw. Eliakimu Maswi, na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Gilbert Mwoga, wamepokelewa leo, Novemba 27, 2026, katika Ofisi Ndogo za TAMISEMI zilizopo Magogoni, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuanza rasmi kutekeleza majukumu yao, kufuatia hafla ya uapisho wa wateule iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kuwasili, Bw. Maswi amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ambapo ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha Ofisi inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, Bw. Maswi amesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na uongozi wa Ofisi katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, hususan kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.

Kwa upande wake, Mhe. Prof. Shemdoe amemsisitiza Katibu Mkuu huyo kuhakikisha maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanatekelezwa kikamilifu na kwa wakati. Aidha, amemtaka kuitisha kikao na Wakuu wa Mikoa tarehe 29 Novemba, 2026 jijini Dodoma mara baada ya kikao cha Mhe. Waziri Mkuu na Wakuu hao wa Mikoa, lengo likiwa kujipanga na kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais na Mhe. Waziri Mkuu katika ngazi za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa.

Ushirikiano huo wa kiutendaji unatarajiwa kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya OWM–TAMISEMI na taasisi zake, ukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa wakati na kwa ufanisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com