Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JUMUIYA YA WAZAZI YAAHIDI KUSIMAMA NA SAMIA,YAAPA KUTOYUMBISHWA NA KAULI ZINAZOKWENDA KINYUME NA MAELEKEZO YAKE



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imesema itaendelea kuwa chombo cha kukisemea, kukinadi na kutetea chama hicho, huku ikisisitiza kuwa haitafuata misimamo mingine nje ya ile inayotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Msimamo huo umetolewa Leo November 27,2026 Jijini hapa na Mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya hiyo Fadhili Maganya wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa Jumuiya ya Wazazi CCM, yakiwamo makatibu wa mikoa na wilaya, yaliyolenga kuwaongezea uwezo wa kiutendaji na kuwajengea ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo amesema watendaji wake hawapaswi kuwa na mzaha katika kulinda na kutetea maslahi ya chama, akisisitiza kuwa jumuiya hiyo itaendelea kumuunga mkono, kumuombea na kumtakia heri mwenyekiti huyo katika uongozi wake.

Amesema, katika kutekeleza wajibu huo, jumuiya itaendelea kuwa mstari wa mbele kukisemea chama na kueneza misimamo yake, akiwataka watendaji kutoyumbishwa na kauli zinazokwenda kinyume na maelekezo ya uongozi wa CCM.

“Jumuiya ya Wazazi itatumika kama kipaza sauti cha kukisemea chama,sisi kama jumuiya tunafuata msimamo wa CCM, tunakinadi na kukitetea,hatutakuwa na mzaha wala woga kwa mtu yeyote anayekwenda kinyume na Chama Cha Mapinduzi,” amesema Maganya.

Amesema jumuiya hiyo itaendelea kusimama na Rais Samia, kumlinda kisiasa, kumuombea na kumtakia heri, akibainisha kuwa haitakuwa tayari kumuaga kabla yeye mwenyewe hajaamua kumaliza safari yake ya uongozi.

“Tutakuwa wa mwisho kumuaga na kumpongeza Rais mpaka pale atakaposema anataka kwenda kupumzika kwake Kizimkazi. Vinginevyo, sisi hatuna kufuata maneno mengine isipokuwa ya Mwenyekiti wetu wa CCM,” alisema.

Kauli hiyo inakuja wakati CCM ikielekea katika uchaguzi wa mwaka ujao, kipindi ambacho jumuiya hiyo inatarajiwa kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kisiasa na kuhamasisha wanachama kuunga mkono misimamo ya chama.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Ali Hapi, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwezo wa watendaji ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya mazingira ya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema mabadiliko makubwa yaliyotokea katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, yakiwamo maendeleo ya teknolojia na kukua kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, yanahitaji viongozi kuendelea kujifunza na kuboresha utendaji wao.

Hapi amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu miiko ya uongozi, matumizi sahihi ya muda wa kazi, mawasiliano, mahusiano na watu pamoja na namna bora ya kuandaa na kuwasilisha taarifa za kiutendaji.

“Tunawaomba muwe tayari kujifunza. Hii ni nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzenu waliofanya vizuri na kutumia uzoefu huo kuboresha maeneo ambayo hatujafanya vizuri,” amesema Hapi.

Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutambua wajibu wao, kuheshimu muda wa kazi na kuzingatia lugha pamoja na mwenendo unaojenga mahusiano mazuri ndani na nje ya jumuiya.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza ubunifu, kuimarisha nidhamu na kuwajengea watendaji uwezo wa kushirikiana na jumuiya nyingine ndani ya chama.

Pamoja na hayo amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili, huku akitaja uandishi bora wa taarifa, mawasiliano na mahusiano ya kikazi kuwa miongoni mwa maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com