Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. SAJAD RAI ATUNUKIWA TUZO YA KIONGOZI BORA SEKTA YA NISHATI


Na Mwandishi Wetu

Meneja Mkazi wa Mansoor Industries Dkt. Sajad Habib Rai ametunukiwa tuzo na Mikono ikimtambua kama mmoja wa viongozi waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya nishati ya mafuta nchini.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo iliyotolewa wakati wa Mkutano wa Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi Jijini Dar es Salaam Novemba 26, 2026 Dkt. Sajad pamoja na mambo mengine ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuisimamia kikamilifu sekta mafuta.

Dkt. Sajad ambaye kwa kiwango kikubwa amewezesha mabadiriko katika sekta hiyo kwa kutoa michango mbalimbali iliyoliwezesha Taifa kupata Mapato kwa kudhibiti aina zote za udanganyifu wa uagizaji na ununuzi wa mafuta kwa ubunifu wake wa mfumo wa udhibiti wa mafuta (BIL), amesema kwake hiyo ni moja ya mambo yanayompa faraja.

"Kikubwa kwangu siku zote nikiwa kama mtaalamu katika sekta hii ya Nishati ya mafuta huwa napenda kuona nchi yangu ikipiga hatua, niliona kuna changamoto ya wizi wa mafuta wakati wa uagizaji na ununuzi jambo lililonifanya kubuni kitu ambacho leo kimeliletea Taifa faida", amesema Dkt. Sajad.

Kimsingi anasisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan imefanya mambo mengi kuhakikisha kama nchi tunapita salama wakati wa changamoto mbalimbali hasa iliyotokana na mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na vita kati ya Marekani na Iran.

Awali Mratibu wa wa 'CEO' Summit Deogratius Kihwele amesema Mkutano huo uliowakutanisha Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali, wawekezaji na watunga sera barani Afrika pamoja na mambo mengine umelenga kuimarisha mifumo ya usalama kwa wawekezaji, kulinda miundombinu ya uwekezaji sanjari na kuweka mikakati ya kudhibiti vihatarishi ili kulinda watu, mali na uwekezaji katika bara la Afrika.

Washiriki walijadili namna taasisi na kampuni zinavyoweza kuacha kuichukulia sekta ya usalama kama gharama za uendeshaji na badala yake kuitambua kama uwekezaji muhimu unaowezesha upanuzi wa biashara, kuongeza imani ya wawekezaji na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.

Aidha, mjadala ulisisitiza umuhimu wa kulinda wafanyakazi, wakandarasi na viongozi wa kampuni wanaotekeleza majukumu yao katika mazingira yenye changamoto za kiusalama, hususan katika sekta za madini, usafirishaji na maendeleo ya miundombinu.

Katika eneo la miundombinu muhimu, washiriki walijadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, waendeshaji wa miundombinu na kampuni binafsi za ulinzi ili kulinda vituo vya nishati, bandari, mitandao ya mawasiliano na mabomba dhidi ya wizi, hujuma na mashambulizi ya kimtandao.

Usalama wa mifumo ya kidijitali pia ulikuwa miongoni mwa mada kuu, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika huduma za benki, biashara na huduma za Serikali. 

Kampuni zilitakiwa kuimarisha uwezo wa kitaalamu, kuandaa mipango madhubuti ya kukabiliana na mashambulizi ya kimtandao na kuhakikisha zina mifumo ya kukabiliana na majanga ya aina hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com