
Na Mwandishi Wetu,Malunde 1 blog- Kahama.
Warembo 15 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga wanatarajiwa kushindana katika kinyang’anyiro cha Miss Shinyanga 2026, kinacholenga kumpata mshindi atakayetangaza utamaduni, vivutio na fursa za kiuchumi zilizopo mkoani humo.
Shindano hilo linatarajiwa kufanyika Oktoba 11, 2026 katika Wilaya ya Kahama, huku mshindi akipata nafasi ya kuwakilisha Shinyanga katika mashindano ya Miss Kanda ya Ziwa yatakayofanyika hivi karibuni na baadaye kushiriki katika jukwaa la Miss Tanzania.
Shindano hilo linaandaliwa na Taasisi ya Holysmile yenye makao makuu yake Kahama mkoani Shinyanga. Taasisi hiyo imewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa ushirikiano na kudhamini shindano hilo ili kufanikisha maandalizi kwa wakati.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Holysmile na Mratibu wa Miss Shinyanga 2026, Arnold Bweichum ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya shindano hilo.
Bweichum amesema mshindi atakuwa na jukumu la kuitangaza Shinyanga kwa kuonyesha utamaduni wake, fursa za kiuchumi na maeneo yanayoweza kuvutia wawekezaji.
“Mpaka sasa tunayo maombi ya washiriki 21 waliojaza fomu, lakini watakaohitajika kushiriki ni 15 pekee. Mchakato wa kupata washiriki unaanza Oktoba 4 hadi 7 na Oktoba 11 ndiyo itakuwa kilele cha kumpata Miss Shinyanga 2026" Amesema.
Aidha, amewataka majaji kuzingatia vigezo na kanuni za mashindano bila upendeleo, akisisitiza kuwa kutowazingatia kunaweza kuathiri taswira ya shindano hilo.
Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mwaita Mwinyimkuu amesema halmashauri hiyo itashirikiana na waandaaji kuhakikisha mchakato wa kumpata Miss Shinyanga unafanyika kwa haki na bila upendeleo.
Amesema mshindi atakuwa na nafasi muhimu ya kutangaza fursa zinazopatikana mkoani Shinyanga ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Nae Mwalimu wa Mitindo na Urembo, Cothbert Kowero amesema waandaaji watazingatia vigezo vya mashindano kuanzia kipindi cha kambi hadi siku ya fainali.
Mmoja wa washiriki wa Miss Shinyanga 2026, Editha Shushu amesema shindano hilo litawapa washiriki fursa ya kujuana, kubadilishana uzoefu na kutambua fursa mbalimbali zilizopo mkoani Shinyanga.
Amesema atatumia nafasi hiyo kuonyesha uwezo wake na kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu fursa za kiuchumi na kiutamaduni zinazopatikana mkoani humo.













Social Plugin