Na Mwandishi Wetu, Shinyanga.
WANANCHI wa Manispaa ya Shinyanga wamepata fursa ya kueleza changamoto mbalimbali za kiusalama zinazowakabili kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, katika mwendelezo wa kampeni ya “Ongea na Kamanda”.
Wananchi hao wamewasilisha changamoto hizo leo, Oktoba 8, 2026, katika Stendi Ndogo iliyopo eneo la Soko Kuu ndani ya Manispaa ya Shinyanga, ambapo Kamanda Magomi alisikiliza maoni, malalamiko na mapendekezo ya wananchi kuhusu masuala ya usalama katika maeneo yao.
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni pamoja na suala la upatikanaji wa leseni za udereva, ambapo baadhi ya madereva walieleza kuwa wanakabiliwa na changamoto kutokana na masharti ya kisheria yanayohitajika kabla ya kupata leseni.
Madereva hao waliomba kuwepo kwa utaratibu wa kuwawezesha kupata mafunzo kupitia vyuo vilivyosajiliwa, ikiwemo mafunzo ya muda mfupi, ili waweze kupata vyeti vinavyohitajika na hatimaye kukidhi masharti ya kupata leseni kwa mujibu wa sheria.
Aidha, wananchi walilalamikia baadhi ya madereva wa pikipiki wanaoendesha kwa fujo, hali ambayo walisema inaweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara pamoja na kusababisha ajali.
Akizungumzia changamoto hiyo, Kamanda Magomi alisema Jeshi la Polisi litakutana na madereva hao kesho kwa ajili ya kuzungumza nao na kuwaelekeza kuhusu wajibu wao wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Kamanda Magomi pia alieleza kuwa baadhi ya madereva hao wamekuwa wakidai kuwa wana vibali mbalimbali, huku taarifa hizo zikitakiwa kufanyiwa uhakiki ili kubaini ukweli wake, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kutumia vibali visivyo halali au kutoa taarifa za kupotosha wananchi.
Changamoto nyingine iliyowasilishwa na wananchi ni kuhusu baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya utapeli, ambapo wananchi waliomba hatua zichukuliwe dhidi ya watu wanaodaiwa kuwahadaa na kuwaingiza katika hasara.
Kamanda Magomi aliwaahidi wananchi kuwa suala hilo litafuatiliwa kwa karibu na Jeshi la Polisi litachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria pale ambapo wahusika watabainika.
Kwa upande wao, wananchi wamepongeza Jeshi la Polisi kwa kutenga muda wa kuwafikia katika maeneo yao, kuwasikiliza na kupokea changamoto zinazowakabili, wakisema hatua hiyo inasaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Kampeni ya “Ongea na Kamanda” ni mpango wa Jeshi la Polisi unaolenga kuwafikia wananchi katika maeneo yao ili kupata fursa ya kuwasilisha changamoto mbalimbali za kiusalama, kutoa maoni na kupendekeza njia za kukabiliana na changamoto hizo.




Social Plugin