Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIMU NI NGUZO YA UTUMISHI WA UMMA NA MAENDELEO YA TAIFA - PROF. SHEMDOE


Na. OWM - TAMISEMI, Bukombe

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe amesema walimu ni nguzo kubwa katika Utumishi wa Umma pamoja na maendeleo ya Taifa, kwani ili nchi iweze kuendelea inahitaji wasomi na wenye jukumu la kuzalisha wasomi ambao wanabobea katika fani mbalimbali ni walimu. 

Prof.  Shemdoe amesemema hayo Oktoba 09, 2026 akiwa Bukombe mkoani Geita wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani Wilaya ya Bukombe kwa mwaka 2026.

“Tuna zaidi ya walimu laki tatu na elfu kumi na mbili katika utumishi wa umma, idadi hiyo ni zaidi ya nusu ya watumishi wote wa umma hivyo walimu ni nguzo kubwa kwenye utumishi na maendeleo ya taifa,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, licha ya kuwa mwalimu ni mlezi lakini ni kielelezo cha maadili na ujenzi wa uwezo wa kizazi kijacho wakiwepo madaktari, wahandisi, wataalam wa kilimo, watafiti, wataalam wa fani mbalimbali pamoja na viongozi katika Utumishi wa Umma na siasa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu Mstaafu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mwalimu umpa mtoto maarifa, umfundisha nidhamu na kuwapa matumaini watoto wanaotoka kwenye familia zenye migogoro.

Ameongeza kuwa, kutokana na jukumu hilo kubwa linalotekelezwa na walimu ndio maana ameratibu siku ya walimu Bukombe ili kuheshimu na kutambua mchango wa walimu na kuongeza kuwa, anatambua walimu ndio wanawezesha kutimiza ndoto za wanafunzi. 

Sherehe za Siku ya Mwalimu Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Oktoba na madhimisho haya yamekuwa yakifanyika Wilayani Bukombe tangu mwaka 2019. Aidha, kwa mwaka huu Kauli Mbiu ya Siku ya Mwalimu Duniani ni “Kusimama na Walimu: Miaka 60 ya kulinda taaluma, kuinua hadhi yake na kuunda mustakabali wetu”.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com