Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIKUNDI 29 KISHAPU VYANUFAIKA NA MKOPO WA ASILIMIA 10 MILIONI 447 AWAMU YA KWANZA MWAKA WA FEHDA 2026/2027



Na Sumai Salum-Kishapu

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amekabidhi mfano wa hundi ya Shilingi milioni 447,422,331 kwa vikundi 29 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Mahitaji Maalumu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi, kukuza mitaji yao na kuimarisha shughuli za uzalishaji mali.


Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo Oktoba 16,2026 katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Mhe. Masindi amesisitiza umuhimu wa wanavikundi kutumia fedha wanazopatiwa kwa malengo yaliyokusudiwa, kuwekeza katika shughuli zenye tija na kusimamia vizuri biashara zao ili ziweze kukua, kuongeza kipato na kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao. Pia amewahimiza kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wengine kunufaika na fursa hiyo.


"Hakikisheni fedha hizi zinatumika kwa shughuli mlizoziomba, kwani mikopo hii ni fursa ya kujikwamua kiuchumi inapaswa kutumiwa kwa umakini na uwajibikaji. Wekeni kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi, kutenganisha fedha za biashara na matumizi binafsi, pamoja na kusimamia miradi yenu kwa ushirikiano ili kuongeza tija na kuhakikisha mikopo inarejeshwa kwa wakati hii siyo Sadaka kumbukeni bali ni mbegu ambayo mnatakiwa kuhakikisha mnaipanda kwenye udingo ulio mzuri na kuimwagilizia ili izae sana nakisha mnufaike,mlipe na wengine waje wachukue" Amesisitiza Masindi


Aidha, amewahimiza wanavikundi kutumia fursa hiyo kukuza mitaji, kuongeza kipato na kutengeneza nafasi za ajira kwa wanachama wengine, akibainisha kuwa mafanikio ya vikundi yatasaidia kuimarisha uchumi wa kaya na kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Kishapu na Taifa kwa ujumla .


Ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira yanayowawezesha wananchi kupata mitaji na kujikwamua kiuchumi. Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kusimamia utekelezaji wa mpango huo na kuendelea kutoa fursa kwa makundi mbalimbali ya wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya kishapu, Mhe. Joel Ndettoson, ameishukuru Serikali kwa kuendeleza mpango wa mikopo inayolenga kuinua uchumi wa wananchi, akibainisha kuwa fursa hiyo ni muhimu katika kukuza biashara, kuongeza ajira na kuimarisha uwezo wa vikundi kujitegemea. Amewataka wanufaika kuwa na mshikamano, uwajibikaji na mipango madhubuti ya matumizi ya fedha ili mikopo hiyo ilete matokeo yaliyokusudiwa.



Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala, amesema ofisi yake itaendelea kutoa elimu na ushauri kwa vikundi kuhusu usimamizi wa fedha, uendeshaji wa biashara na matumizi sahihi ya mikopo. Ameeleza kuwa ufuatiliaji wa shughuli za vikundi ni muhimu ili kuhakikisha fedha zinatumika kwa malengo yaliyowasilishwa na kurejeshwa kwa wakati.


Akizungumza kwa niaba ya kikundi cha Wanawake cha Jembe la Bibi kutoka Kata ya Mwadui Lohumbo, Tarafa ya Mondo, mwakilishi wa kikundi hicho ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa ya kupata mtaji wa kuendeleza shughuli zao za kiuchumi. Amesema wanatarajia kutumia fedha hizo kuboresha shughuli zao za uzalishaji na kuongeza kipato cha wanachama pamoja na familia zao.


Naye mwakilishi wa kikundi cha Vijana cha Mchongomani kutoka Kata ya Kishapu, Tarafa ya Kishapu, ameeleza kuwa mikopo hiyo ni fursa ya vijana kujiajiri, kukuza shughuli zao za biashara na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira. Kwa upande wake, Julius Mpuya, mwakilishi wa kundi la Watu Wenye Mahitaji Maalumu kutoka Kata ya Talaga, Tarafa ya Negezi, ameishukuru Serikali kwa kuwajumuisha katika mpango huo, akisema msaada huo utawapa nafasi ya kuimarisha shughuli zao na kuongeza uwezo wa kujitegemea.



Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu kiuchumi kupitia fursa za mitaji na mikopo, huku ushirikiano kati ya Serikali, Halmashauri na wanufaika ukiwa muhimu katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa tija, zinakuza biashara na kuchangia maendeleo endelevu ya wananchi wa Wilaya ya Kishapu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, akizungumza wakati akikabidhi mfano wa hundi ya Shilingi milioni 447,422,331 kwa vikundi 29 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Mahitaji Maalumu Wilayani humo Oktoba 16,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Fatma Mohamed, akizungumza wakati Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi akikabidhi mfano wa hundi ya Shilingi milioni 447,422,331 kwa vikundi 29 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Mahitaji Maalumu Wilayani humo Oktoba 16,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya kishapu, Mhe. Joel Ndettoson, akizungumza wakati Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi akikabidhi mfano wa hundi ya Shilingi milioni 447,422,331 kwa vikundi 29 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Mahitaji Maalumu Wilayani humo Oktoba 16,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala, akizungumza wakati Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi akikabidhi mfano wa hundi ya Shilingi milioni 447,422,331 kwa vikundi 29 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Mahitaji Maalumu Wilayani humo Oktoba 16,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com