NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Kupata cheti cha kimataifa cha ubora cha ISO 9001:2015 kumeiwezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuweka mkakati wa kutumia teknolojia kupunguza muda wa kutuma fedha za mikopo kwa wanafunzi wanaostahili kutoka siku moja au mbili hadi sekunde mbili.
Akizungumza leo wakati wa hafla ya kukabidhiwa cheti hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema bodi hiyo inapanga kuunganisha mifumo yake na kampuni za simu za mkononi ili kuwawezesha wanafunzi kupokea fedha zao papo hapo baada ya taratibu zinazohitajika kukamilika.
Amesema kwa sasa bodi hiyo hutuma fedha ndani ya siku moja au mbili baada ya kukamilika kwa taratibu zote, lakini inalenga kuboresha zaidi huduma hiyo kwa kutumia mifumo ya kidijitali.
“Kwa sasa tunatuma fedha ndani ya siku moja au mbili baada ya taratibu zote kukamilika. Hata hivyo, haturidhishwi na muda huo. Tunataka kuunganisha mifumo yetu na kampuni za simu ili wanafunzi waweze kupokea fedha zao papo hapo, ndani ya sekunde mbili,” amesema Dkt. Kiwia.
Amesema HESLB imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia, ambapo wanafunzi sasa wanaweza kuomba mikopo, kuhakiki taarifa zao, kufuatilia akaunti na kuhamisha fedha kwa kutumia simu janja.
Amefafanua kuwa hali hiyo ni tofauti na zamani ambapo bodi ilitegemea taratibu za karatasi zilizohitaji maandalizi makubwa katika zoezi la uombaji mikopo, huku akiongeza kuwa mifumo ya HESLB tayari imeunganishwa na majukwaa ya benki ili kurahisisha huduma.
Dkt. Kiwia amesema bodi hiyo imewasaidia wanafunzi zaidi ya milioni moja nchini kwa kutoa mikopo yenye thamani ya karibu Sh trilioni tisa, akieleza kuwa fedha hizo ni uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu.
Amesema uwekezaji huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya taifa kwa kuwa unawawezesha Watanzania kupata elimu ya juu na kuongeza ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali za uchumi.
“Sh trilioni tisa ni kiasi kinachoweza kulinganishwa na uwekezaji katika Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), lakini uwekezaji wetu ni katika rasilimali watu,” amesema.
Amesema cheti hicho ni cha kwanza kwa HESLB na kinatarajiwa kuimarisha imani ya wanafunzi, taasisi za elimu ya juu, Serikali na wadau wengine kuhusu ubora, uwazi na ufanisi wa huduma zinazotolewa na bodi hiyo.
Ameongeza kuwa cheti hicho kinahusisha makao makuu ya HESLB, ofisi ya Zanzibar na ofisi za kanda za Arusha, Mbeya, Mwanza na Mtwara, hatua inayolenga kuhakikisha taratibu za usimamizi wa ubora zinafuatwa katika maeneo yote ya utendaji.
Aidha, amesema bodi hiyo imeanza maandalizi ya kupata cheti cha ISO 27001 kinachohusu usimamizi wa usalama wa taarifa, huku ikipanga pia kufuata ISO 37001 kinachohusu mifumo ya usimamizi wa kupambana na rushwa.
Amesisitiza kuwa kudumisha cheti cha ubora kunahitaji ushiriki wa menejimenti na watumishi wote, ufuatiliaji wa mara kwa mara wa utendaji na maboresho yanayotokana na maoni ya wanufaika wa huduma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, ameipongeza HESLB kwa kupata cheti hicho, akisema kitasaidia kuimarisha mifumo ya taasisi na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma.
Amesema kupata cheti ni hatua ya mwanzo, huku kukidumisha kukihitaji taasisi kuendelea kutimiza matakwa ya kiwango husika, kufuatilia utendaji na kuhakikisha mifumo yake inafanya kazi kwa ufanisi.
“Kupata cheti ni hatua moja, lakini kukidumisha ni hatua nyingine. Lazima muendelee kutimiza matakwa yake, kufuatilia utendaji na kuhakikisha mifumo inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema Dkt. Katunzi.
Ameeleza kuwa kiwango cha ISO 9001:2015 kinatumika katika taasisi za aina na ukubwa tofauti kwa lengo la kuboresha kuridhika kwa wateja, kuongeza tija na kuimarisha ufanisi wa kiutendaji.
Amesema kiwango hicho ni muhimu kwa HESLB kutokana na jukumu lake la kubaini wanafunzi wanaostahili mikopo na kusimamia utoaji wa fedha hizo kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, jambo linalohitaji mifumo inayohakikisha uwazi na uaminifu.
Dkt. Katunzi amehimiza HESLB kuendelea kutafuta vyeti vingine vya kimataifa, huku akizitaka taasisi za umma na binafsi kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa ili kuboresha huduma na kuimarisha weledi.
Amesema juhudi hizo zinaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhimiza ufanisi, weledi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin