Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI NYANSAHO AWATAKA VIJANA KUJENGA UZALENDO, NIDHAMU NA UWEZO WA KUJITEGEMEA




Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amewataka vijana nchini kuimarisha uzalendo, nidhamu, ubunifu na uwezo wa kujitegemea kiuchumi, akisisitiza kuwa maendeleo na usalama wa Taifa vinahitaji ushiriki wa kila mwananchi.

Amesema vijana wanapaswa kutumia elimu waliyoipata kutambua fursa zilizopo, kuanzisha shughuli za uzalishaji mali na kujenga uwezo wa kutatua changamoto zinazolikabili Taifa, badala ya kutegemea ajira pekee baada ya kuhitimu masomo.

Dkt. Nyansaho ametoa wito huo Novemba 14, 2026, alipokuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya Kidato cha Sita ya Shule ya Wasichana Canossa, iliyopo Tegeta Kibaoni, jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, amesisitiza umuhimu wa elimu katika kuwawezesha wanawake na wasichana kutambua uwezo wao, kukuza vipaji na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii na Taifa.

Ameipongeza shule hiyo kwa kutimiza miaka 20 ya kutoa elimu na kuwalea mabinti katika misingi ya imani, maadili, nidhamu na uwajibikaji, akieleza kuwa falsafa ya kumjenga mtoto wa kike kiroho, kitaaluma na kimaadili ni msingi muhimu wa kuandaa wanawake wenye uwezo wa kushiriki katika uongozi na maendeleo ya nchi.

Amesema mafanikio ya wahitimu hao yanaakisi hatua zilizopigwa na Tanzania katika kupanua fursa za elimu na uwezeshaji wa wanawake.

Akitolea mfano wa nafasi ya wanawake katika uongozi, ametaja kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Machi 19, 2021, kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini, akisema hatua hiyo inaonesha uwezekano wa wanawake kushika nafasi za juu za uongozi na kushiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa.

Amewahimiza wahitimu kuendelea kujenga uwezo wao kupitia elimu, bidii, nidhamu, uadilifu na uthubutu, akisisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania yanahitaji mchango wa kila Mtanzania bila kujali jinsia.

Katika eneo la ulinzi na usalama, Dkt. Nyansaho amesema jukumu la kulinda amani, umoja na mshikamano wa nchi si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi.

Amefafanua kuwa uzalendo wa kweli unaonekana katika matendo ya kila siku, yakiwamo kuheshimu sheria, kupinga rushwa, kulinda mali za umma na mazingira, kujiepusha na vitendo vya uhalifu na kushiriki katika kudumisha umoja wa kitaifa.

Aidha, amewataka vijana kuwa kizazi chenye maarifa ya kisasa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia kutatua changamoto za maendeleo, akibainisha kuwa amani ni msingi wa maendeleo endelevu na inapaswa kulindwa na kila mmoja.

Kuhusu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Waziri huyo amewahimiza wahitimu kuwa tayari kushiriki katika mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali.

Amesema mafunzo ya JKT yana nafasi muhimu katika kuwajengea vijana uzalendo, nidhamu, uongozi, stadi za kazi, uwezo wa kushirikiana na kujitegemea.

Vilevile, amewataka wahitimu kuyatazama mafunzo hayo kama fursa ya kujijenga kimwili, kiakili na kimaadili, pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia kuishi na kushirikiana na vijana kutoka maeneo na mazingira mbalimbali ya nchi.

Akizungumzia suala la kujitegemea kiuchumi, Dkt. Nyansaho amewataka vijana kutokuweka matumaini yao katika ajira pekee, bali wajifunze kutambua na kutumia fursa zinazowazunguka.

Amesema vijana wanaweza kutumia maarifa na teknolojia kuanzisha biashara, shughuli za uzalishaji mali na miradi mbalimbali itakayowawezesha kujipatia kipato na kutengeneza ajira kwa wengine.

Ameongeza kuwa Tanzania inahitaji vijana wenye maarifa, ubunifu, maadili mema na uwezo wa kujitegemea kiuchumi ili kuchangia ustawi wa jamii na kuimarisha usalama wa Taifa kwa muda mrefu.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com