Na. Mwandishi Wetu - Maputo, Msumbiji
TANZANIA imejipambanua Kimataifa katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa kwa kuwekeza katika mifumo ya tahadhari za mapema, uratibu wa kitaasisi na mikakati ya kifedha inayolenga kupunguza athari za majanga na kujenga ustahimilivu wa jamii.
Hatua hizo zimeelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kapsar Mmuya, aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, katika Kongamano la Kimataifa la Kupunguza Hatari za Maafa na Kuimarisha Ustahimilivu wa Bara la Afrika Dhidi ya Majanga, lililofanyika kuanzia Oktoba 13 hadi 15, 2026, jijini Maputo, Msumbiji.
Mmuya amesema Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), inaendelea kukabiliwa na ongezeko la majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi, vihatarishi vingine vya asili na shughuli za kibinadamu, yakiwemo mafuriko, ukame, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya mlipuko, moto, ajali na vimbunga.
Amesema majanga hayo yanaathiri maisha ya wananchi, miundombinu, huduma za kijamii na uchumi wa taifa, hali inayolazimu kuimarishwa kwa mifumo ya kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa.
“Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa maafa kwa kuzingatia Mfumo wa Sendai wa Umoja wa Mataifa wa Kupunguza Hatari za Maafa wa mwaka 2015–2030, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Ajenda ya Afrika 2063 na mikakati mingine ya kikanda na kimataifa,” amesema Mhe. Mmuya.
Amesema Tanzania pia inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati inayochangia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, ulioanzishwa kwa msukumo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha, amesema Tanzania imejumuisha makundi maalumu, yakiwemo wanawake, vijana, wazee, watu waliokimbia makazi yao na watu wenye ulemavu, katika sera na sheria za usimamizi wa maafa ili kuhakikisha yanashiriki katika mipango ya matumizi ya ardhi, ujenzi wa miundombinu na programu za kujenga ustahimilivu.
Katika eneo la ufadhili, Mhe. Mmuya amesema Tanzania inaunga mkono ongezeko la hatua kwa hatua la fedha za ndani kwa ajili ya kupunguza hatari za maafa na kujiandaa kukabiliana nayo, sambamba na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali hizo.
“Tanzania inaendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa na mifumo ya mawasiliano kuanzia ngazi ya taifa hadi jamii, huku ikibadili mwelekeo kutoka kutoa tahadhari pekee kwenda kuchukua hatua za mapema kabla ya kutokea kwa athari za maafa,” amesema.
Kuhusu El Niño, Mmuya amesema Tanzania imezindua Mpango wa Taifa wa Dharura waEl Niño na Hatua za Mapema wa mwaka 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha maandalizi na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kongamano la Kimataifa la Usimamizi wa Maafa limefanikiwa kuwaleta pamoja viongozi, watunga sera, na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na jumuiya za kikanda ili kujadili mbinu za kupunguza hatari za majanga pamoja na kuchochea mabadiliko ya kimkakati ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari za ukame na kupunguza hatari za maafa barani Afrika.

Social Plugin