Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SH5 BILIONI KUINUA KAMPUNI CHANGA ZA TEHAMA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

SERIKALI imeweka Sh5 bilioni kupitia Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wabunifu wanaomiliki kampuni changa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwa ni hatua inayolenga kubadili mawazo na bunifu za kiteknolojia kuwa biashara, ajira na fursa za masoko.

Programu hiyo ya Uwezeshaji wa Mikopo kwa Kampuni Changa za TEHAMA imezinduliwa jana, Oktoba 2, 2026, jijini Dodoma, huku Serikali ikisisitiza kuwa mafanikio yake hayatapimwa kwa kiasi cha fedha kitakachotolewa pekee, bali kwa matokeo yatakayopatikana kwa kampuni zitakazonufaika.

Akizindua programu hiyo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, alisema Serikali inalenga kuhakikisha mitaji hiyo inasaidia kampuni changa kukua, kuzalisha ajira, kuongeza mauzo na mapato, pamoja na kufungua masoko mapya ndani na nje ya Tanzania.

“Swali letu si tu tumetoa mikopo kiasi gani? Swali muhimu zaidi ni fedha hizo zimeleta mabadiliko gani?” alisema.

Alisema mikopo hiyo itatolewa katika madaraja matatu, kuanzia Sh1 milioni hadi Sh25 milioni, zaidi ya Sh25 milioni hadi Sh50 milioni, na zaidi ya Sh50 milioni hadi Sh100 milioni, kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.

Kairuki alisema programu hiyo inalenga kampuni zinazotengeneza suluhisho za kidijitali katika sekta mbalimbali za uchumi, zikiwamo teknolojia za fedha, kilimo, utalii, elimu, bima, usafirishaji na ugavi, pamoja na biashara mtandao.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, utekelezaji wa programu hiyo utafanyika kwa ushirikiano na Benki ya Azania, huku makubaliano ya ushirikiano kati ya pande hizo yakisainiwa wakati wa hafla hiyo.


MATOKEO YA SH5 BILIONI

Kairuki alisema Serikali haitaki programu hiyo kuishia katika utoaji wa mikopo, bali inataka kufuatilia namna fedha hizo zinavyobadili biashara za wanufaika.

Alisema viashiria vitakavyotumika kupima mafanikio ni pamoja na idadi ya kampuni zitakazokua, ajira zitakazozalishwa, ongezeko la mauzo na mapato, bidhaa na huduma mpya zitakazoingia sokoni, upanuzi wa masoko na kiwango cha urejeshaji wa mikopo.

Kwa mantiki hiyo, kampuni zitakazonufaika zitatakiwa kutumia fedha hizo kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili kuongeza uwezo wa biashara na kuifanya iwe endelevu.

Waziri huyo pia alielekeza kuwekwa kwa mfumo maalumu wa kufuatilia na kupima matokeo ya programu hiyo, kwa kushirikisha Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tume ya TEHAMA na Benki ya Azania.

Mfumo huo utasaidia kufuatilia mwenendo wa kampuni wanufaika pamoja na matokeo ya mikopo katika maeneo ya ajira, mauzo, masoko, bidhaa na huduma mpya na urejeshaji wa fedha.

KAMPUNI CHANGA NA SOKO LA SERIKALI

Mbali na mtaji, Serikali imeweka mkazo katika kuongeza fursa za masoko kwa kampuni changa za TEHAMA.

Kairuki ameielekeza Tume ya TEHAMA kukamilisha mwongozo utakaowezesha kampuni hizo kushiriki katika zabuni za Serikali na kuwasilisha mwongozo huo kwa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa hatua zinazostahili.

Hatua hiyo inalenga kuongeza nafasi kwa kampuni changa kupata masoko kupitia ununuzi wa Serikali, badala ya kutegemea mtaji pekee kama msingi wa ukuaji wa biashara.

Waziri pia ameelekeza kuandaliwa kwa mpango wa elimu kwa umma utakaowasaidia wabunifu na kampuni changa kuelewa vigezo vya kupata mikopo, taratibu za maombi, wajibu wa wanufaika na namna ya kutumia fursa hiyo.

CHANGAMOTO YA MTAJI

Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya TEHAMA, Dk. Henry Mwanyika, alisema kampuni changa zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya mtaji, huku baadhi ya benki zikisita kuwekeza katika biashara hizo kutokana na hatari zinazohusishwa nazo.

Alisema upatikanaji wa mikopo unaweza kusaidia kampuni changa kupata nafasi ya kukuza mawazo na bidhaa zao, huku akiwataka wanufaika kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati.

Mwanyika alisisitiza kuwa fedha hizo si ruzuku wala sadaka, bali ni mikopo ambayo urejeshaji wake utasaidia kuwafungulia fursa wabunifu wengine.


AZANIA YAWEKA MKAZO KWENYE UWEZO

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dk. Esther Mang’enya, alisema benki hiyo kwa kushirikiana na Wizara itahusika katika mchakato wa tathmini na utoaji wa mikopo kwa kampuni zitakazokidhi vigezo.

Alisema ushirikiano huo hauishii katika kutoa fedha, bali pia unahusisha kuwajengea vijana uwezo katika usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu na uandaaji wa mipango ya biashara.

Kwa mujibu wa Mang’enya, hatua hiyo inalenga kusaidia kujenga kampuni zenye uwezo wa kuendelea na shughuli zao, kuzalisha ajira na kukua kibiashara.
WABUNIFU WATAKIWA KUANGALIA SEKTA 21

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga, alisema uwekezaji huo unalenga kuwawezesha vijana kushiriki katika kukuza uchumi wa kidijitali kupitia bidhaa, viwanda vya kidijitali na sekta mahiri.

Aliwataka wabunifu kuelekeza teknolojia katika sekta zote 21 za uchumi ili kuongeza mchango wa ubunifu katika maendeleo ya Taifa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahoro Muhaji, alisema programu hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendeleza kampuni changa na sekta ya ubunifu.

Alisema Sh5 bilioni ni mwanzo muhimu wa kuongeza wigo wa uwezeshaji, akibainisha kuwa awali fursa za ushindani wa ubunifu zilikuwa zikitoa zawadi za hadi Sh50 milioni.

Kwa upande wake, wawakilishi wa sekta ya kampuni changa wamewataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa umakini na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kuwafikia wabunifu wengine.

Programu hiyo inaweka mkazo katika kuunganisha mtaji, ubunifu, ujuzi na soko, huku Serikali ikitarajia kampuni changa za TEHAMA kutumia fursa hiyo kujenga biashara zenye uwezo wa kukua, kuzalisha ajira na kuongeza mchango wa uchumi wa kidijitali katika maendeleo ya Tanzania.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com