CHAMA cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT) kimesema kinaendelea na mikakati ya kuimarisha uandishi wa habari unaozipa nafasi changamoto, mahitaji na mafanikio ya wananchi wa vijijini, ili kuhakikisha taarifa zinazowahusu zinapata uzito unaostahili katika vyombo vya habari.
Katibu wa RUJAT Prosper Kwigize amesema Chama hicho bado kina changamoto ya baadhi ya vyombo vya habari kuzipa kipaumbele habari zinazotoka mijini, huku taarifa muhimu zinazohusu maisha ya wananchi wa vijijini zikikosa nafasi ya kutosha, hali inayo athiri ushiriki wao katika mijadala na maamuzi yanayohusu maendeleo.
Akizungumza leo Oktoba 31,2026 Jijini Dodoma kwenye Kongamano na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama hicho, amesema wazo la kuanzishwa kwa chama hicho lilitokana na kujifunza mifumo ya vyama vya waandishi wa habari za vijijini katika nchi nyingine za Afrika, hususan India na Afrika Kusini.
Amesema wazo hilo lilianza mwaka 2020 na baadaye waandishi wa habari 20 kutoka mikoa mbalimbali walikutana Dodoma na kukubaliana kuanzisha chama hicho, hatua iliyofuatwa na kuandaliwa kwa katiba na kuanza kwa taratibu za usajili.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, mchakato huo uliwezeshwa na wadau mbalimbali, ikiwemo Idara ya Habari Maelezo iliyotoa barua ya mapendekezo kwa Msajili wa Vyama, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na uongozi wa kituo cha Dodoma FM uliowapatia ukumbi na huduma ya intaneti kwa ajili ya vikao vya maandalizi.
Amesema RUJAT ambayo ilianza na wanachama 20 sasa ina wanachama 120, huku ikiwa na maombi zaidi ya 60 kutoka kwa waandishi wengine wanaotaka kujiunga, jambo alilolitaja kuwa ishara ya kuongezeka kwa mwitikio wa waandishi kuhusu umuhimu wa kuimarisha uandishi wa habari za vijijini.
Amesisitiza kuwa dhamira ya chama hicho si kuongeza idadi ya wanachama pekee, bali kuhakikisha habari zinazotoka maeneo ya vijijini zinapata nafasi katika majukwaa mbalimbali na kuondoa mtazamo unaoweza kufanya taarifa za mijini kuonekana kuwa na thamani kubwa kuliko zile za vijijini.
Ametoa mfano wa kutegemeana kati ya maisha ya maeneo ya mijini na vijijini, akisema miji haiwezi kujitegemea bila uzalishaji wa chakula kutoka maeneo ya uzalishaji, hivyo ni muhimu changamoto na mchango wa wananchi wa vijijini kupewa nafasi katika mijadala ya kitaifa.
Amesema chama hicho kinaamini jamii yenye taarifa sahihi ina uwezo mkubwa zaidi wa kufanya maamuzi yanayohusu maisha na maendeleo yake kuliko jamii isiyopata taarifa.
Katika kutekeleza dhamira hiyo, amesema RUJAT imeweka mkazo katika kujenga uwezo wa wanachama, kuzalisha habari zenye matokeo, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kufanya utetezi wa uhuru wa habari, upatikanaji wa taarifa na usawa wa kijinsia.
Kuhusu matumizi ya teknolojia, amesema mabadiliko kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali yamefungua fursa mpya kwa waandishi wa habari, lakini yanahitaji matumizi yenye weledi ili kuhakikisha maudhui yanayochapishwa yanachochea mijadala na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Ameonya kuwa baadhi ya waandishi wanaojitegemea wanakabiliwa na changamoto ya kufanya kazi zote za uandishi, uhariri, utangazaji na uongozi wa vyombo vyao kwa wakati mmoja, hali inayoweza kuathiri ubora wa kazi zao.
Amesema RUJAT pia inalenga kuimarisha uandishi wa habari wenye matokeo badala ya kuridhika na kuchapisha au kutangaza taarifa bila kufuatilia kama zimeleta mabadiliko kwa wananchi.
Katika eneo la usawa wa kijinsia, amesema chama hicho kinataka mjadala huo upanuliwe zaidi ya changamoto zinazowakabili waandishi wa habari wanawake, na kujumuisha pia hali ya wanawake na wasichana wa vijijini ambao wakati mwingine hawapati huduma na taarifa zinazowahusu kutokana na uhaba wa habari zinazotoka katika maeneo yao.
Aidha, amesema RUJAT imekuwa ikitumia mtandao wake wa wanachama kutoka mikoa mbalimbali kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya waandishi, kuanzia Songea hadi Mara na Kigoma hadi Rufiji.
Amebainisha kuwa chama hicho pia kinapanga kuanzisha tuzo maalumu za kutambua waandishi wanaofanya kazi bora katika kuripoti masuala ya vijijini, ambazo zinatarajiwa kuanza mwaka 2027 endapo mipango na ushirikiano na wadau vitafanikiwa.
Kwigize amesema tuzo hizo hazitazingatia tu mahali anapoishi mwandishi, bali ubora wa kazi zake, matumizi ya vyanzo vya habari kutoka vijijini na nafasi anayoipa jamii katika habari anazozalisha.
Amefafanua kuwa mwandishi hatatambuliwa kuwa amefanya uandishi wa habari za vijijini kwa kuandika taarifa za mikutano au matamko ya viongozi pekee, bali anapaswa kwenda katika jamii, kusikiliza wananchi na kuchunguza hali halisi ya maisha yao.
Katika kuonyesha utekelezaji wa majukumu yake, amesema RUJAT imekuwa ikiendesha mijadala, mikutano na shughuli za kujenga uwezo kwa wanachama, huku ikishirikiana na wadau mbalimbali wa habari na maendeleo.
Katibu huyo alisema RUJAT itaendelea kushirikiana na wanachama na wadau wa habari kuhakikisha uandishi wa habari za vijijini unakuwa jukwaa muhimu la kuibua changamoto, kutetea maslahi ya wananchi na kuonesha fursa za maendeleo, akisisitiza kuwa sauti za wananchi wa vijijini zinapaswa kusikika na kupewa nafasi katika mijadala inayounda mustakabali wa taifa.


TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin