Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSIGWA ATAKA UTAFITI KUBAINI KWA NINI WANANCHI WANAPOTEZA IMANI NA VYOMBO VYA HABARI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akizungumza wakati wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), jijini Dodoma, Oktoba 31, 2026. Picha na Kadama Malunde
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akizungumza wakati wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), jijini Dodoma, Oktoba 31, 2026. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akizungumza wakati wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), jijini Dodoma, Oktoba 31, 2026. 

Na Dotto Kwilasa, Dodoma 

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ameeleza wasiwasi wake kuhusu kupungua kwa ushawishi wa waandishi wa habari kwa wananchi, akitaka kufanyika kwa utafiti kubaini sababu zinazowafanya wananchi kupunguza ufuatiliaji wa vyombo vya habari na kuelekeza imani yao katika makundi mengine yasiyo na jukumu la kitaaluma la kuhabarisha umma.

Amesema hali hiyo ni ishara inayopaswa kuitafakari tasnia ya habari nchini kwa kuwa jukumu la kuhabarisha jamii linapaswa kutekelezwa na wanahabari wenye weledi, wanaozingatia maadili na misingi ya kutopendelea upande wowote.

Msigwa ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 31, 2026, jijini Dodoma, wakati wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), akisisitiza kuwa waandishi wanapaswa kurejesha nafasi yao kama sauti ya wananchi na kusimamia maslahi mapana ya jamii.

Ameonya kuwa ikiwa waandishi wataendelea  kuruhusu makundi yenye ajenda ovu kuchukua nafasi ya taaluma ya habari, watapoteza umuhimu wao katika jamii na kuwanyima wananchi haki ya kupata taarifa zinazowasilisha maslahi yao kwa usawa.

Katika kulinda nafasi hiyo, Msigwa amesema tofauti ya mwanaharakati na mwandishi wa habari ni kwamba mwanaharakati anaweza kusimamia ajenda maalumu, wakati mwanahabari anapaswa kuangalia maslahi ya wananchi kwa ujumla bila kuongozwa na matakwa yake binafsi.

Ametolea mfano wanaharakati wa mazingira, demokrasia na uchumi, akisema kila kundi linaweza kusimamia eneo lake hata pale ambapo maslahi hayo yanakinzana na mahitaji ya baadhi ya wananchi.

"Waandishi wa habari ni sauti ya wananchi,mwanahabari anaangalia maslahi ya wananchi bila kuangalia yeye mwandishi anataka nini," amesema.

Msigwa amehusisha pia changamoto hiyo na uwiano wa upatikanaji wa habari kati ya mijini na vijijini, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanaishi vijijini, lakini sehemu kubwa ya vyombo vya habari imejikita mijini na hivyo kuwanyima watu wa pembezoni kusikika.

Amesema hali hiyo inachangia wananchi wengi wa vijijini kukosa uwakilishi wa kutosha katika maudhui yanayotolewa na vyombo vya habari, hivyo kutoa wito kwa RUJAT kufanya utafiti na kuweka mikakati ya kuziba pengo hilo.

Katika hatua nyingine, amewataka wanahabari kutambua wajibu wao wa kulinda taifa kupitia kalamu zao, akieleza kuwa taarifa zimekuwa nyenzo muhimu katika migogoro ya dunia na zinaweza kutumiwa kujenga au kudhoofisha mataifa.

Katika kuunga mkono juhudi za chama hicho, Msigwa aliahidi kutoa Sh milioni 10 kwa RUJAT kwa ajili ya kuimarisha shughuli zake na kuwawezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amesema chama hicho kinalenga kuboresha uandishi wa habari za vijijini kwa kuhakikisha waandishi hawaishii kuripoti taarifa za mikutano na matamko ya viongozi, bali wanachunguza namna matukio na miradi mbalimbali inavyoathiri maisha ya wananchi.

Amesema Uandishi wa habari za vijijini unapaswa kuwa na sura ya watu, akitolea mfano ujenzi wa barabara ya kilomita 100 kutoka Morogoro hadi Chalinze, ambapo mwandishi anapaswa kuchunguza manufaa na athari zake kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Meena amesema chama hicho pia kinahitaji kuwekeza katika mafunzo ya waandishi kuhusu uandishi wa habari za vijijini, matumizi ya teknolojia na akili unde (AI), ili kuongeza ubora na upekee wa habari zinazozalishwa.

Naye Katibu wa RUJAT Prosper Kwigize  amesema chama hicho kimekua kutoka wanachama waanzilishi 20 mwaka 2020 hadi kufikia wanachama 120, huku kikiwa na maombi zaidi ya 60 ya waandishi wanaotaka kujiunga.

Amesema RUJAT inalenga kuhakikisha habari ambazo hazijaripotiwa vya kutosha kutoka vijijini zinapata nafasi katika majukwaa ya habari, kwa kuwa jamii yenye taarifa sahihi inaweza kufanya maamuzi bora kuhusu maendeleo yake.

Ameongeza kuwa chama hicho kimepanga kuanzisha tuzo maalumu za uandishi wa habari za vijijini mwaka 2027 ili kutambua waandishi wanaozalisha habari zenye kina na matokeo kwa jamii.

Naye Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, ambaye pia ni mwandishi wa habari kitaaluma, ametaka wanahabari kurejesha ubora wa uandishi wa habari kwa kuimarisha uchunguzi, ubunifu na ushindani wa kitaaluma.

Bulaya amesema baadhi ya waandishi wamekuwa wakitegemea taarifa wanazopewa na viongozi badala ya kufanya mahojiano na uchunguzi wa kina, hali inayopunguza upekee na ubora wa habari.

Amesema uzoefu wa zamani ulionesha ushindani mkubwa wa kitaaluma, ambapo waandishi walijitahidi kupata habari za kipekee badala ya kuridhika na taarifa zilizokuwa zikitolewa na vyanzo rasmi.

Ametumia nafasi hiyo kuwashauri  waandishi kutumia ubunifu kuibua masuala yanayogusa maisha ya wananchi, akitolea mfano wa habari za uchunguzi alizowahi kufanya kuhusu watoto chini ya miaka 14 kuingia katika vilabu vya starehe nyakati za usiku bila uangalizi unaostahili.

Bulaya ameahidi kuendelea kushirikiana na wanahabari katika kutetea maslahi yao na kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com