Na Dotto Kwilasa ,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua majengo ya ofisi za Wizara 26, Taasisi 11 za Serikali na mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026.
Uzinduzi huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa mradi wa Mji wa Serikali Mtumba, unaolenga kuziweka ofisi za Serikali katika eneo moja lenye miundombinu ya kisasa na mazingira yanayorahisisha utendaji kazi.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alitoa taarifa hiyo jana jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.
Msigwa alisema uzinduzi huo uliokuwa umeahirishwa kufuatia kifo cha mume wa Rais, sasa utafanyika Oktoba 30 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, Septemba 6, 2026, kukamilika kwa miundombinu hiyo kunatarajiwa kuwezesha watumishi 18,510 kufanya kazi ndani ya Mji wa Serikali Mtumba.
WATUMISHI 18,510 KUNUFAIKA
Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba umetekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilianza Novemba 28, 2018, kwa ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za muda yaliyokamilika Machi 22, 2019.
Awamu ya pili ilianza Oktoba 2021, ikilenga kujenga majengo ya kudumu ya Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na miundombinu inayohitajika kuwezesha shughuli za kiutawala.
Mradi huo umehusisha ujenzi wa majengo ya ofisi, barabara, mifumo ya umeme, maji, mawasiliano na huduma nyingine muhimu kwa matumizi ya watumishi na taasisi zitakazofanya kazi katika eneo hilo.
Kwa upande wa barabara, jumla ya kilomita 57.1 za barabara za lami zimejengwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji ndani ya mji huo.
UMEME, MAJI NA TEHAMA
Mji wa Serikali Mtumba umeendelezwa kwa kuzingatia dhana ya mji janja (Smart City), inayolenga kutumia teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma na uendeshaji wa shughuli za kila siku.
Katika sekta ya nishati, mradi unahusisha miundombinu ya kusambaza umeme chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42, kwa lengo la kuhudumia majengo na maeneo mbalimbali ya mji huo.
Pia, mifumo ya maji safi na uondoshaji wa maji taka ni sehemu ya miundombinu inayolenga kukidhi mahitaji ya watumishi na shughuli za ofisi.
Katika eneo la teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), mifumo ya kisasa inawekwa ili kurahisisha mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa baina ya ofisi za Serikali.
Aidha, mifumo ya kamera za usalama (CCTV) ni sehemu ya miundombinu inayolenga kuimarisha ulinzi wa majengo na maeneo ya Mji wa Serikali.
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ni miongoni mwa taasisi zinazohusika na kazi za uwekaji wa mifumo ya umeme, TEHAMA, viyoyozi, lifti na vifaa vingine vya kielektroniki katika baadhi ya majengo yaliyopo Mtumba.
MIUNDOMBINU YA KIJANI
Mbali na majengo na barabara, Mji wa Serikali Mtumba unahusisha miundombinu mingine, ikiwemo Uwanja wa Mashujaa, kituo cha zimamoto na mifumo ya mifereji ya maji.
Mipango ya maendeleo ya eneo hilo pia imejumuisha vipengele vya uhifadhi wa mazingira, kama vile upandaji miti, matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua na uboreshaji wa mandhari.
Hatua hizo zinalenga kuweka mazingira yanayokidhi mahitaji ya kazi huku yakizingatia matumizi endelevu ya rasilimali na utunzaji wa mazingira.
DODOMA KUIMARISHA HADHI YAKE
Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha shughuli za kiutawala jijini Dodoma, kwa kuunganisha Wizara na Taasisi mbalimbali katika eneo moja.
Kuwepo kwa ofisi hizo katika eneo lenye miundombinu ya pamoja kunatarajiwa kurahisisha uratibu wa shughuli za Serikali na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.
Aidha, uwepo wa watumishi na taasisi hizo unatarajiwa kuongeza mahitaji ya huduma mbalimbali, hatua inayoweza kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yanayozunguka Mji wa Serikali.
Uzinduzi wa Oktoba 30, 2026, unatarajiwa kuweka alama nyingine katika maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba, ambao ni sehemu ya mpango wa kuimarisha Dodoma kama kitovu cha shughuli za Serikali nchini.




TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin