Na Sheila Ahmadi, kigoma
WAZIRI wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaendelea katika maeneo mbalimbali mkoani kigoma ambapo kuna mradi unaondelea kwenye daraja la Malagarasi ambapo kazi za awali za ujenzi wa madaraja na miundombinu mingine zimeanza licha ya kuwepo kwa madai kuwa hakuna kazi zinazoendelea kufanyika.
Ukaguzi uliofanyika katika maeneo ya mradi umeonesha kuwa wakandarasi wanaendelea kutekeleza majukumu yao ikiwemo kujenga misingi ya madaraja, makaravati ya sanduku (box culverts) na kuweka mabomba ya kupitisha maji hatua muhimu katika maandalizi ya miundombinu ya reli hiyo.
Aidha Profesa Mbarawa ameongeza kuwa kukamilika kwa kazi hizo za awali kutaiwezesha Serikali na wakandarasi kuingia katika hatua zinazofuata za ujenzi ikiwemo kuinua na kukamilisha madaraja pamoja na miundombinu mingine itakayohakikisha reli inafanya kazi kwa ufanisi na usalama.
Serikali kupitia Wizara ya uchukuzi inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kumwezesha mkandarasi kutekeleza kazi kwa mwendelezo unaotakiwa akisisitiza kuwa suala la fedha linaendelea kupewa kipaumbele ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi.
“Tunataka kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha na tunampa mkandarasi fedha kadiri anavyohitaji ili aweze kukamilisha mradi huu vizuri,” amesema Profesa Mbarawa huku akieleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kazi zinaendelea na mradi unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.
Vilevile Ziara zilizofanyika sehemu mbalimbali za mradi zikiwemo Lot 3 na Lot 6 ambapo zimeonesha hatua zinazochukuliwa na wakandarasi katika kutekeleza ujenzi huku Lot 6 ikiwa imeanza utekelezaji wake katika kipindi cha hivi karibuni hivyo hatua hizo zinaonesha umuhimu wa kufuatilia maendeleo ya kila kipande ili kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati.
Profesa Mbarawa amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maono na usimamizi wa miradi ya maendeleo ya reli nchini na uwekezaji unaofanywa na Serikali unalenga kuimarisha miundombinu ya usafiri, kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo na kuongeza fursa za kiuchumi katika maeneo yatakayohudumiwa na reli hiyo.
Pia kukamilika kwa reli ya kisasa ya SGR katika kipande kinachounganisha Dar es Salaam na Kigoma kutaboresha huduma za usafiri huku treni zikitarajiwa kuendeshwa kwa kasi ya hadi kilomita 160 kwa saa. Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia maendeleo ya mradi hadi ukamilike kwa viwango vinavyotakiwa ili wananchi wanufaike na huduma bora za usafiri na taifa lipate chachu mpya ya maendeleo ya kiuchumi.





TAFUTA HABARI
Social Plugin