Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YAIMARISHA UKAGUZI WA BIDHAA ZA VIPODOZI, VYAKULA KATAVI


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), Kanda ya Magharibi, limeimarisha ukaguzi wa bidhaa za vipodozi na vyakula katika Mkoa wa Katavi kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinakidhi viwango vya ubora na usalama kwa afya za watumiaji.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo lililoanza Oktoba 19 hadi 25 mwaka huu, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TBS, Peter Musiba, alisema ukaguzi huo ulilenga wauzaji wa bidhaa za vipodozi, vyakula pamoja na wafungashaji wa bidhaa za chakula zikiwemo mchele, unga, mikate na mafuta ya kupikia.

Alisema katika ukaguzi huo, TBS imeendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kuondoa sokoni bidhaa za vipodozi visivyosajiliwa, vyenye viambata sumu na vilivyokwisha muda wa matumizi, pamoja na bidhaa nyingine zisizokidhi matakwa ya viwango.

Musiba alisema elimu inayoendelea kutolewa imechangia kupungua kwa bidhaa zisizokidhi viwango sokoni, ingawa bado kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaokutwa na bidhaa zisizo salama.

Alitoa wito kwa wazalishaji na wauzaji wa vipodozi na vyakula kuhakikisha wanasajili maeneo yao ya biashara na kutekeleza matakwa ya TBS, huku wazalishaji na wafungashaji wa bidhaa za chakula wakitakiwa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kabla ya kuziingiza sokoni.

Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya za watumiaji na kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Kuhusu Mkoa wa Katavi, Musiba alisema kuna zaidi ya wafanyabiashara 3,000 wa vipodozi na vyakula, huku TBS ikiendelea na zoezi la kutoa elimu na kusajili maeneo ya biashara ili kuhakikisha wafanyabiashara wote wanapata vibali vinavyotakiwa.

Aliongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wachache wa vipodozi bado hawajatekeleza matakwa ya usajili, hali aliyosema inachangiwa kwa kiasi na uelewa mdogo kuhusu taratibu za TBS.

Alisema shirika hilo litaendelea kuwafikia wafanyabiashara hao kwa mazungumzo na elimu ili kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuuza vipodozi salama na vinavyokidhi viwango.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa vipodozi na vyakula katika Manispaa ya Mpanda, Mwanise Mwakilema, alisema kupata kibali cha TBS kumemsaidia kuendesha biashara yake kwa uelewa wa taratibu zinazopaswa kufuatwa.

Mwakilema alisema tangu aanze biashara hiyo, amekuwa akishirikiana na TBS na kupata maelekezo kuhusu namna bora ya kuendesha biashara yake.

Alisema wafanyabiashara wanapaswa kuichukulia TBS kama mshirika muhimu wa biashara zao kwa kuwa, mbali na kusimamia viwango, shirika hilo hutoa elimu inayowawezesha kufanya biashara kwa kuzingatia usalama wa bidhaa na afya za watumiaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com