Na Mwandishi Wetu, Serengeti
WAZAZI na walezi wametakiwa kuwalea watoto katika mazingira salama, yenye upendo, heshima na mawasiliano mazuri, pamoja na kuwafundisha kutambua vitendo vya ukatili na unyanyasaji.
Wito huo umetolewa Oktoba 19, 2026, na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Emmanuel Kisiri, ambaye ni Polisi wa Kata ya Ikoma, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, alipotembelea familia ya Thomas Thomas katika Kijiji cha Parknyigoti.
Kisiri amesema ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji huanzia nyumbani kupitia malezi bora yanayotolewa na wazazi na walezi.
Amesema ni muhimu watoto kupewa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili bila hofu, hatua itakayowasaidia wazazi na walezi kubaini mapema viashiria vya ukatili na kuchukua hatua zinazofaa.
Aidha, ameitaka jamii kutambua kuwa malezi bora na ulinzi wa watoto si jukumu la wazazi pekee, bali ni wajibu wa kila mwanajamii kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira yenye usalama, haki na upendo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuzuia ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto na kuhakikisha wanapata fursa ya kukua na kuendelezwa katika mazingira salama.

.jpeg)

TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin