Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda, akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamdun, wakati wa Kongamano la MISA TAN Wadau 2026 jijini Mwanza. Picha na Kadama Malunde.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda, akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamdun, wakati wa Kongamano la MISA TAN Wadau 2026 jijini Mwanza.
Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, akizungumza wakati wa Kongamano la MISA TAN Wadau 2026 lililofanyika jijini Mwanza.
Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, akizungumza wakati wa Kongamano la MISA TAN Wadau 2026 lililofanyika jijini Mwanza.
Sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria Kongamano la MISA TAN Wadau 2026 lililofanyika jijini Mwanza.
Sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria Kongamano la MISA TAN Wadau 2026 lililofanyika jijini Mwanza.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA Tanzania), imefanya kongamano na wadau kutoka taasisi za umma na sekta binafsi jijini Mwanza kwa lengo la kujadili namna ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa sekta mbalimbali na maendeleo ya Tanzania kupitia uandishi wa habari.
Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika Oktoba 12, 2026, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, CP Salum Hamdun, ameipongeza MISA Tanzania kwa kuwakutanisha wadau na kusisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kuhabarisha umma kuhusu fursa za kiuchumi, mipango ya Serikali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Machunda amesema Mkoa wa Mwanza una fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kutumika kikamilifu kuchochea uwekezaji na kuongeza kipato cha wananchi, akizitaja sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, utalii, madini, usafirishaji na viwanda kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa za maendeleo.
Amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kuzitangaza fursa hizo kwa lugha inayoeleweka ili kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali, wakiwemo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, wafanyabiashara na wawekezaji.
Aidha, amezitaka taasisi za umma kuimarisha mawasiliano na wanahabari kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mipango, miradi, mafanikio na changamoto za utekelezaji, akieleza kuwa hatua hiyo itaongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha uwajibikaji.
Machunda amesisitiza pia umuhimu wa ushirikiano unaozingatia kuheshimiana, kuaminiana na kutambua majukumu ya kila upande, huku vyombo vya habari vikiendelea kuzingatia weledi na maadili ya taaluma katika ukusanyaji na usambazaji wa taarifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amevitaka vyombo vya habari nchini kuandika na kuripoti habari zenye tija zinazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku vikizingatia ukweli, weledi na maadili ya taaluma ya habari.
Soko amesema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kuelimisha jamii na kuchangia maendeleo ya nchi, akiwataka kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha taarifa wanazochapisha au kurusha zimethibitishwa ili kuepusha upotoshaji na uchonganishi katika jamii.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhuru wa kiuchumi wa vyombo vya habari ili viweze kujiendesha kwa uendelevu, kuboresha huduma zake na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila kuathiri uhuru wa uhariri.
Kongamano hilo limeongozwa na kaulimbiu “Uhuru wa Vyombo vya Habari Kiuchumi” na kuwakutanisha wanachama 60 wa MISA Tanzania kutoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kati, pamoja na wadau mbalimbali kutoka taasisi za umma na sekta binafsi.
Kanda ya Ziwa inajumuisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera; Kanda ya Magharibi inajumuisha Kigoma, Tabora na Katavi; huku Kanda ya Kati ikijumuisha Singida na Dodoma.
Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki ni Idara ya Uhamiaji, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), pamoja na wadau wengine.





















































































































Social Plugin