Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIRADI YA WORLD VISIONI YAPONGEZWA NA DC KISHAPU


Mkuu wa Wilaya ya mkoani Shinyanga Mhe Peter Masindi akiwa ndiye Mwenyekiti wa kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision wilayani humo Oktoba 19, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.


Na Sumai Salum-Kishapu


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amesema Shirika la World Vision Tanzania limeendelea kuwa mshirika wa Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya maji safi na salama, afya, lishe, usafi wa mazingira na uwezeshaji wa kiuchumi.


Masindi ameyasema hayo wakati wa Kikao cha Uratibu wa Utekelezaji wa Miradi ya World Vision wilayani Kishapu, kilicholenga kutathmini mafanikio, matumizi ya bajeti, changamoto na mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa miradi hiyo ili wananchi wanufaike na huduma zinazotolewa.

Mkuu wa Wilaya ya mkoani Shinyanga Mhe Peter Masindi akiwa ndiye Mwenyekiti wa kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision wilayani humo Oktoba 19, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya


Amesema ushirikiano kati ya Serikali na mashirika ya maendeleo una mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa huduma za kijamii na kuinua uchumi wa wananchi, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, umoja na matumizi sahihi ya rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya miradi.


“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji. Ninawakaribisha wadau na wawekezaji kutoka mashirika mbalimbali kuja kuwekeza nchini, hususan Kishapu, kwa sababu wananchi wake ni wachapakazi na wana uwezo wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo,” amesema Masindi.

Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed akizungumza kwenye kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision wilayani humo Oktoba 19,2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.


Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuimarisha umoja kwa kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali ili kuunganisha nguvu, mawazo na rasilimali zao, akieleza kuwa ushirikiano huo unaweza kuwasaidia kutekeleza shughuli kubwa zaidi za kiuchumi na kuboresha kipato cha familia zao.


Kwa upande wake, Meneja wa World Vision Kanda ya Ziwa, Goodluck Nnko, ameeleza kuwa shirika hilo linaendelea kutekeleza programu za maendeleo kwa kushirikiana na Serikali na jamii, zikilenga kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi katika maeneo mbalimbali.

Meneja mradi WorldVision Kanda ya Ziwa Goodluck Nnko akizungumza kwenye kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Oktoba 19,2026 Katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi


Akielezea utekelezaji wa miradi katika maeneo ya Lagana na Mwakipoya, Mratibu wa Miradi ya Maendeleo wa World Vision Kishapu, Yohana Masanja, amesema shirika hilo limechangia upatikanaji wa maji safi na salama kupitia miradi mikubwa mitatu iliyotekelezwa katika vijiji vya Mwakipoya, Iboja na Belwdi.


Amesema kila mradi wa maji umegharimu shilingi milioni 79, fedha zilizotolewa kutoka nchini Canada, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza changamoto ya umbali unaotumiwa na wananchi, hususan wanawake, kutafuta maji na kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya nyumbani.


“Lengo la miradi hii ni kumsaidia mwanamke kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji safi na salama, huku tukiendelea kushirikiana na Serikali na jamii kuhakikisha huduma hiyo inachangia kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Masanja.

Mratibu wa mradi ya maendeleo Lagana na Mwakipoya AP, WorldVision wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Yohana Masanja akiwasilisha mada kwenye kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision kilichofanyika wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Oktoba 19,2026 Katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi


Ameeleza pia kuwa miradi hiyo imekuwa ikihamasisha jamii kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na kunawa mikono katika nyakati muhimu ili kuzuia magonjwa yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira, yakiwemo magonjwa ya kuhara na kipindupindu. Aidha, amesema koki 3,750 zimesambazwa kwa kaya katika maeneo ya mradi kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa maji na kuboresha usafi wa nyumbani.


Katika upande wa uwezeshaji wa kiuchumi, Masanja amesema zaidi ya vikundi 457 vya hisa vimeundwa na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali, zikiwemo ufugaji wa nyuki, mbuzi na kuku pamoja na kilimo cha umwagiliaji, hatua inayolenga kuongeza kipato na kuimarisha uwezo wa familia kujitegemea kiuchumi.


Katika sekta ya kilimo, taarifa za utekelezaji zimeeleza kuwa Lagana AP imeimarisha matumizi ya teknolojia za kilimo kwa kusambaza pampu 50 za maji na vinyunyizio vinne kwa ajili ya kurahisisha umwagiliaji wa mazao ya bustani na viazi lishe.


Naye Mratibu wa Mradi wa NOURISH, Jackline Kawiche, ameelezea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwaka 2027,mradi ambao umejikita zaidi katika kuboresha mifumo ya kupambana na udumavu, kuongeza kipato cha kaya na ustahimilivu wa jamii kukabiliana na majanga huku akisisitiza umuhimu wa kufuatilia shughuli zilizobaki ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kabla ya mradi kuhitimishwa.

Meneja mradi wa Nourish Mkoani Shinyanga Jackline Kawiche akiwasilisha mada kwenye kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Oktoba 19,2026 Katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi


Kwa upande wa Mradi wa Grow Enrich, Meneja wa mradi huo, Shukrani Dickson, amesema awamu ya pili ya utekelezaji ilianza mwaka 2023 na inatarajiwa kukamilika mwaka 2027, ikiwa na lengo la kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto. Ameeleza kuwa takribani asilimia 70 ya mradi huo unaweka mkazo katika kuongeza virutubisho kwenye chakula ili kuboresha lishe, hususan kwa wanawake wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.


Wadau wengine, wakiwemo Kivulini, VisionFund na Recoda, wanaendelea kuwa sehemu ya jitihada za maendeleo kupitia maeneo yao ya utekelezaji, kwa kuzingatia majukumu na programu zao.


Ushirikiano kati ya Serikali, World Vision na mashirika mengine ya maendeleo unaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha huduma za maji, afya, lishe, usafi wa mazingira na uzalishaji mali. Kwa kuunganisha rasilimali, utaalamu na nguvu za jamii, wadau hao wanaweza kuongeza ufanisi wa miradi na kuchochea maendeleo endelevu yatakayoboresha maisha ya wananchi wa Kishapu.

Meneja Mradi wa Grow Enrich Shukran Dickson akizungumza kwenye kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Oktoba 19, 2026 Katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi
Afisa Mradi VisionFund Stanley Mgaya akielezea huduma za kifedha kwa vikundi na Kaya

Afisa Mradi kutoka Shirika la RECODA Josephine Joseph akielezea mchango katika programu matokeo na nafasi yake
Meneja Mradi wa KIVULINI akizungumza kwenye kikao Cha Uratibu wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la WorldVision wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Oktoba 19, 2026 Katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi



























































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com